powered by
send-it.me

Adventist World-Kiswahili inamshukuru kila aliyejiandikisha kwa ajili ya jarida hilo, kupitia kwa jukwaa letu la awali, yaani chaneli ya WhatsApp. Tumefurahia kupokea jumbe kutoka kwako, na vilevile shuhuda za jinsi umetumia jarida hili linalotia moyo kuwafikia wengine kwa ajili ya Kristo!

Tungependa ujue kuwa tulihamia jukwaa jipya tangu Februari 2024. Zaidi ya yote, tungependa uhame pamoja nasi. Adventist World-Kiswahili haitaki kumwacha nyuma yeyote aliyejiandikisha.

 

Badala ya kupokea ujumbe wa WhatsApp pamoja na toleo jipya kila mwezi, sasa tunakupa kiungo kwa tovuti ya bure ambayo ni nzuri kwa simu, ambapo unaweza kuyasoma makala yote, kama kawaida. 

Pia tutakiweka kiungo hicho kwenye ukurasa wa Facebook wa Adventist World-Kiswahili kila mwezi, ambapo unaweza kututumia jumbe na taarifa kuhusu jinsi makala hii inakufaidi wewe na jamii yako. Unaweza kututumia maoni na mapendekezo jinsi ya kuifanya makala hii iwafae zaidi wasomaji!

Ukipenda, unaweza kutuma baruapepe: 
kwambokaj@ecd.adventist.org ukiwa na maswali yoyote.

 

Moja ya manufaa ya tovuti mpya ya Adventist World-Kiswahili ambayo ni nzuri kwa simu, ni

kwamba kutakuwa na lugha zingine nyingi za kuchagua, ikiwa ungependelea Kiingereza au lugha nyingine yoyote, unaweza kuangalia kama ipo, kando na ile ya kawaida ya Kiswahili.

 

Manufaa mengine ni kwamba ni rahisi kushiriki kiungo hicho kipya cha Adventist World-Kiswahili, kwa marafiki na familia. Tunakuhimiza ufanye hivyo. Hebu kiangalie sasa hivi.

 

Tunatumai kuwa na uhusiano mrefu na wa furaha na wasomaji wetu wa Adventist World-Kiswahili.

 

Mungu akubariki,

 

Timu ya Adventist World-Kiswahili

Tunaamini katika nguvu ya maombi, na tunakaribisha hitaji la maombi ambayo tutashiriki katika ibada ya watendakazi kila Jumatano asubuhi. Tuma maombi yako kwa kwambokaj@ecd.adventist.org, na utuombee tunapofanya kazi pamoja kuendeleza ufalme wa Mungu.

 

Picha ya jalada: sezer66 / iStock / Getty Images Plus  / Getty Images 

Je, umegundua kuenea kwa roho ya kutoridhika siku hizi?

 

Wengi wanatafuta yale ambayo hatimaye yatatosheleza matamanio yao, lakini wanakuta kwamba kadiri wanavyopata zaidi, ndivyo wanavyotaka zaidi.

 

Sehemu kubwa ya mgogoro katika ulimwengu huu unahusu watu kung’ang’ania kwa ubinafsi au uchu wa utajiri, cheo na mamlaka.

 

Kwa kuwa sisi ni binadamu wapotevu, mwelekeo wetu ni wa ubinafsi, kinyume kabisa na tabia ya Mungu ya upendo kamili, usio na ubinafsi. Dhambi na ubinafsi huenda pamoja.

 

Katika mazingira fulani, neno “dhambi” halisikiki sana tena. Wengine hawapendelei kuongea kuhusu dhambi, wakipendelea jumbe chanya tu.

 

Biblia, hata hivyo, ina mengi ya kusema kuhusu dhambi, ikiwa ni pamoja na katika Amri Kumi. Miongoni mwake iko amri ya kumi dhidi ya kutamani, inayozidi kupuuzwa (Kut. 20:17).

 

Kusikia kuhusu dhambi ya kutamani ni nadra sana siku hizi. Kwa kweli, ikiwa ungeuliza watu barabarani kutamani ni nini, nashangaa wangapi leo hii hata wangeweza kujua maana ya neno hilo.

 

Kwa ufupi, dhambi ya kutamani inajumuisha ubinafsi, kutojizuia kutamani kile kinachomilikiwa na wengine.

 

Cha kusikitisha, mengi yanayotuzunguka yametengenezwa ili kutufanya tutamani kwa njia hii—kujisikia utupu na shauku ya kuwa na tusivyonavyo na mara nyingine kutamani yale yanayomilikiwa na wengine. Kutoka katika matangazo ya kawaida hadi kwa taratibu za mitandao ya kijamii na zaidi, tunashambuliwa na jumbe zisizokoma zikielekeza akili zetu kwa ubinafsi, kutoridhika, kutamani vitu vingi tusivyovihitaji au tunavyohitaji. Paulo, kwa upande mwingine, anatuambia tuwe wenye kuridhika na hali yoyote itupatayo (Flp. 4:12).

 

Bila shaka, ikiwa tutakuwa waaminifu sisi wenyewe, haitachukua kampeni za matangazo mazuri au taratibu za mitandao ya kijamii kutufanya tutamani. Sisi sote tu wazuri sana katika hilo.

 

Kwa njia nyingi, kutamani ni dhambi iliyosahauliwa sana siku hizi. Na, labda, hilo halishangazi, kwa sababu imeunganishwa sana na asili ya dhambi—wakati Lusifa alianguka, alijawa na kiburi na uchu wa kupandishwa hadi kwenye kiti cha enzi cha Mungu. Kinyume kabisa na mwovu, Yesu alifanya kinyume cha uchu wa cheo na mamlaka—kujishusha ili kuwa binadamu na kufa kwa ajili yetu (tazama Flp. 2:5-8).

 

Na katika Kristo, kuna habari njema sana kwetu.

 

Kusudi kuu la msisitizo wa Maandiko kuhusu dhambi ni ahadi kwamba tunaweza kupata ushindi kupitia Kristo na hatimaye, kupitia kazi ya Kristo, dhambi zote, uovu, mateso na kifo vitaondolewa.

 

Ikiwa tutaweka imani yetu katika Kristo, tutagundua kwamba shauku zetu kuu, ambazo hakuna kitu katika ulimwengu huu wa sasa kinachoweza kutosheleza kabisa, zitatimizwa milele katika ufalme Wake ujao. Na, hata sasa, tunaweza kupata kuridhika na amani tele katika Yeye (Flp. 4:7).

 

Kwa wakati huu, na tumwombe Mungu atubadilishe mioyo yetu na atusaidie kufuata mfano wa mwisho wa upendo usio na ubinafsi uliotolewa na Yesu—mwanzilishi na mtimizaji wa imani yetu (Ebr. 12:2), ambaye alitupenda na kujitoa kwa ajili yetu (Efe. 5:2).

Kwa Siku ya Vijana Duniani, Machi 16, vijana Waadventista wa Sabato wa Peru walisambaza vibao vilivyohusu upendo wa Mungu katika barabara kuu na vivuko vya wanaotembea kwa miguu.

"Jibu lilikuwa zuri sana, na tunabarikiwa sana na msaada, uaminifu, na kujitoa kwa dada zetu wanapoitikia wito wa Mungu kwenda na kuufikia ulimwengu."

– Oyuntuya Batsukh, mkurugenzi wa huduma za wanawake wa Misheni ya Mongolia, kuhusu safari maalum ya utume wa wanawake katika mwezi wa Machi. Kikundi cha wanawake kutoka makanisa kadhaa ya Waadventista katika mji mkuu wa Ulaanbaatar kilisafiri umbali wa takribani kilomita 435 kwenda Uvurkhangai. Huko walitembelea shule na taasisi za serikali, kutoa msaada wa kiafya na kufanya semina za afya. Ufikiaji wao haukujifunga kwa elimu ya afya pekee; pia waligawa nakala 140 za kitabu cha Ellen G. White, The Great Controversy.

“Katika siku hizi, tunawalea watoto bila kutambua jukumu lao katika huduma za familia na kijamii. Kozi hii inasisitiza umuhimu wa watoto katika jamii. . . . Kuwafundisha mbinu za huduma ya kwanza huwawezesha kuchukua hatua katika hali za kushindwa kupumua, kifafa, na kukoma kwa kupumua na moyo. Zaidi ya kuokoa maisha, mwongozo huu huamsha ndani yao hamu ya kufuata taaluma katika eneo la afya.”

– José Guataçara, daktari mtaalamu wa upasuaji wa mifupa na matibabu ya majeraha, kuhusu mafunzo ya huduma ya kwanza yaliyotolewa kwa watoto yaliyoanzishwa na Hospitali ya Waadventista ya Belém huko Pará, kaskazini mwa Brazili. Zaidi ya watoto 34 walipewa cheti cha kumaliza mafunzo wakati wa sherehe maalum mwezi Machi katika vituo vya taasisi ya huduma za afya. Wakati wa mafunzo, washiriki vijana walijifunza mbinu muhimu kama vile kuokoa moyo na mapafu (CPR), kudhibiti kutoka kwa damu, na kufunga viungo, vitu ambavyo ni muhimu katika kusaidia kesi za dharura.

“[Siku 100 za maombi] ni mkakati wa kuhamasisha nchi nzima katika kutafuta ulinzi na mwongozo wa Bwana katika utoaji wa PNG kwa Kristo na mipango ya kliniki kuu ya afya.”

– Malachi Yani, mwenyekiti wa Union Misheni ya Papua New Guinea, kuhusu jitihada hiyo ambayo ni sehemu ya maandalizi ya kusukuma uinjilisti ulioanza mwishoni mwa Aprili na unaofika hadi Mei. Zaidi ya wahubiri 200 kutoka Kusini mwa Pasifiki wanashiriki katika PNG kwa Kristo ambayo inafanyika katika maeneo 2,000.

Miaka 75

Mwezi wa Machi, huduma ya redio ya Your Story Hour ilisherehekea kumbukumbu yake ya miaka 75. Mwaka 1949, Your Story Hour iliwasilisha hadithi yao ya kwanza kwenye kituo kimoja cha redio kilichoitwa WHFB, ambacho kilikuwa katika Benton Harbor, Michigan, Marekani. Imegeuka kuwa kipindi cha kila wiki kinachopeperushwa kwenye maelfu ya vituo vya redio ulimwenguni kote. Maigizo ya sauti yanayofaa kwa familia huleta hadithi za kuvutia zilizo na msingi katika Biblia, mashujaa wa kihistoria, wamishonari, miujiza ya kisasa, na safari za kisasa ambazo hufundisha thamani za Kikristo na sifa za tabia chanya. Huduma ilianza awali kama wakati wa hadithi kwa watoto siku ya Jumamosi mchana karibu na kituo cha zimamoto. Hatimaye ikawa maarufu sana hivi kwamba H.M.S. Richards, mwanzilishi wa huduma ya redio ya Voice of Prophecy, alisikia kuhusu hiyo na kupendekeza kushiriki hadithi hizi na watoto zaidi kupitia redio.

“Kwa njia hii tunaweza kuwafikia wale wanaohitaji zaidi, tukiwapa rasilimali zitakazowawezeha kukua. Na watu pia wataweza kupata uangalizi wa bure wa meno popote wanapoishi.”

—Fabio Salles, mkurugenzi wa Shirika la Waadventista la Maendeleo na Misaada (ADRA) nchini Brazili, kuhusu ushirikiano kati ya Idara ya Leba na ADRA Brazili, kununua basi la afya. Lengo la mkakati huo ni kukuza afya bora na fursa za ushirikiano kwa watu wenye mahitaji katika Brasilia. Basi hilo litasafiri huko Brasilia na litawasaidia watu kupata kazi na pia kutoa uangalizi wa bure wa meno.

Zaidi ya watu 300

Idadi ya wanajamii huko Detroit, Michigan, Marekani, waliopokea huduma muhimu za matibabu na meno. Zaidi ya waliojitolea na wataalamu 200 walishiriki katika Mtandao wa Uinjilisti wa Matibabu wa Waadventista uliodhaminiwa na Konferensi za Mikoa ya Ziwa na Michigan. Changamoto kubwa ambayo waandaaji wa tukio hilo walikabiliana nayo ilikuwa kupata mamia ya watu wa kujitolea na wataalamu wa matibabu ili kufanikisha tukio hilo. Kwa bahati nzuri, miezi kadhaa kabla ya kliniki hiyo ya siku moja, viongozi kutoka konferensi zote mbili waliandaa mkutano wa maombi uliolenga kuunganisha makanisa, kuangazia changamoto za jiji na jamii inayozunguka, na hatimaye kuwafanya washiriki kujitolea kwa kliniki ya matibabu.

"Mungu ametuita kuwa waombezi. Divisheni ya Kaskazini mwa Asia-Pasifiki na Unioni Konferensi ya Korea wamepewa  jukumu kubwa: 'Uinjilisti wa Dirisha la 10/40.' ”

– Kim Sun Hwan, mkurugenzi wa Utume wa Waadventista wa Divisheni ya Kaskazini mwa Asia-Pasifiki, wakati wa Mkutano wa Kimataifa wa Uinjilisti wa 10/40 uliofanyika katika kanisa la Chuo Kikuu cha Sahmyook huko Korea Kusini. Mkutano huo ulifanyika kuanzia Machi 14-16, na mbali na kuwa na mawasilisho mbalimbali pia ulijumuisha ushuhuda kutoka kwa wamishonari wa Waadventista wanaohudumu katika dirisha la 10/40

Zaidi ya 530

Idadi ya vijana waliokusanyika katika Taasisi ya Waadventista ya Cruzeiro do Sul (IACS) huko Taquara, Rio Grande do Sul, Brazili, kushiriki katika mafunzo ya mradi wa "Gideon’s 300". Lengo la mradi huo ni kuwapa vijana mafunzo ya kufundisha masomo ya Biblia, kudumisha imani ya vijana hao na kuwashirikisha katika misheni ya kufundisha na kuandaa kizazi kinachowaza kuhusu misheni. Mbali na vijana 530 katika IACS, tukio hilo lilijumuisha washiriki 120 katika jiji la Passo Fundo.

Kwa moyo wa huruma na kujitolea, Huduma ya Taarifa za Wakristo (Christian Record Services [CRS]) inaendelea kusimama imara huku ikisherehekea kipindi kirefu cha ajabu — Miaka 125 ya kujitoa kikamilifu katika kuwatumikia watu duniani kote ambao ni vipofu na wasioona vizuri. Tangu kuanzishwa kwake mwaka 1899, CRS, huduma ya Divisheni ya Amerika Kaskazini ya Waadventista wa Sabato, imekuwa nguzo ya tumaini, ikivunja vizuizi na kutoa huduma za kubadilisha maisha kwa watu wanaokabiliana na changamoto za kuona.

 

Ikianzishwa kwa misingi ya upendo na maadili ya Kikristo, CRS inajitahidi kukidhi mahitaji yanayobadilika ya wanachama wake, viongozi wa huduma yake walisisitiza. “Kwa zaidi ya karne moja, shirika hili limekuwa mstari wa mbele katika jitihada za kuwawezesha watu vipofu au wasioona vizuri, kukuza ushirikishwaji na kuwezesha kujitegemea,” walisema.

 

Maadhimisho ya miaka 125 si tu sherehe ya urefu, bali ni ushahidi wa mabadiliko endelevu ambayo CRS imekuwa nayo na inaendelea kuwa nayo katika maisha ya watu wasiohesabika.

 

“Mwanzilishi wa shirika hili, Austin O. Wilson, alitamani kuwepo kwa rasilimali zaidi za Breli (mfumo wa maandishi yenye vidutu yatumiwayo na vipofu) za Kikristo kwa watu kama yeye mwenyewe ili kujifunza zaidi kuhusu upendo wa Mungu kwao,” Mwenyekiti wa CRS Diane Thurber alisema kutoka makao makuu ya shirika huko Lincoln, Nebraska, Marekani. “Kufikia hatua hii kubwa sana kunadhihirisha jinsi wazo lake lilivyotimizwa na huduma na programu zilizozidi kupanuliwa kwa miaka. Tunatarajia ukuaji endelevu na huduma yenye maana.”

 

Huku CRS ikiadhimisha Miaka 125 ya huduma, viongozi walisema kuwa huduma hiyo inasimama kama mfano wenye kung’aa wa upendo, uthabiti na nguvu yenye kubadilisha ya huduma iliyojitolea wakati ikiendelea kuiangazia njia kuelekea ulimwengu unaojumuisha zaidi na unaofikiwa kwa urahisi kwa jamii ya vipofu na wasioona vizuri.

 

 

KUHUSU AUSTIN O. WILSON NA KAZI YA CRS

Mnamo mwaka 1899, Austin O. Wilson, kijana asiyeona vizuri akiwa katika miaka yake ya mwanzo ya 20, alikuwa na wasiwasi kuhusu ukosefu wa vifaa vya kusomea vya Kikristo vinavyopatikana kwa ajili ya vipofu. Akaamua kufanya jaribio. Akichukua guruto la nguo, alilibadilisha ili liweze kutoshea vigogo viwili vya chuma vilivyokuwa na bamba za karatasi nzito kati yao. Wakati vigogo hivyo vilipobana kwenye guruto, alama zilizoinuka kwenye vigogo hivyo ziliacha alama kwenye karatasi, kuzalisha ukurasa mmoja wa gazeti la Breli aliloliita Christian Record. Zaidi ya miaka mia moja baadaye, Christian Record bado linaendelea kuchapishwa, pamoja na magazeti mengine nane.

Wilson alizalisha nakala 75 za Christian Record ya kwanza. Katika miaka ya 1920, Christian Record ilikuwa ikifikishwa mikononi mwa maelfu ya watu vipofu ulimwenguni kote.

 

Mnamo 1933 na 1934, Huduma za Taarifa za Wakristo zilikuwa mojawapo ya waonyeshaji katika Ukumbi wa Dini katika Maonyesho ya Ulimwengu, chini ya kauli mbiu “Karne ya Maendeleo,” huko Chicago, Illinois, Marekani. Mwaka mmoja baadaye, CRS ilionyeshwa tena kwa umaarufu katika Ukumbi wa Sayansi katika Maonyesho ya Marekani, yaliyofanyika San Diego, California.

 

Mnamo 1950, vitabu vya kusomwa kwa sauti vilirekodiwa kwa mara ya kwanza kwa Huduma za Taarifa za Wakristo. Sasa kuna zaidi ya vitabu vya kusomwa kwa sauti 1,600 vinavyopatikana kupitia Maktaba ya Naomi Chapman Turner kwa ajili ya watu walio Vipofu.

 

Mnamo 1967, Makambi ya Kitaifa kwa Watoto Vipofu yalikuwa yameanzishwa. Msimu wa kwanza wa joto, kambi hilo lilifanyika Florida na vijana 23 walihudhuria. Tangu wakati huo, programu hii ya ufikiaji imekuwa ikitoa karibu uzoefu wa kujenga ujasiri 50,000 katika mazingira ya asili kupitia makambi haya maalum.

Divisheni ya Waadventista wa Sabato ya Amerika Kati (IAD) ilizindua maktaba yake mpya ya mtandaoni iliyopewa jina jipya la Adventist Virtual Library (BiVA) kwa mamia ya shule na vyuo vikuu katika mfumo wake wote wa elimu wakati wa sherehe ya moja kwa moja ya mtandaoni iliyofanyika kutokea Alajuela, Costa Rica, tarehe 4 mwezi Machi. Idadi kubwa ya wanafunzi, walimu, waelimishaji, viongozi wa kanisa, na wasimamizi walikusanyika katika Chuo Kikuu cha Waadventista cha Amerika ya Kati ili kushuhudia namna mpya ya kuwasiliana na mfumo, chapa, na nyenzo zilizopo.

 

BiVA ya IAD, chombo cha huduma kinachoongozwa na idara ya elimu ya Divisheni, kilianzishwa kwa mara ya kwanza mwaka 2007. Lengo lake ni kusaidia nyenzo za maktaba na kuimarisha tabia ya utafiti, kujifunza, na kusoma kwa wanafunzi wa umri wote katika mipaka yote ya Divisheni.

 

 

TOVUTI, MUUNDO, NA NEMBO MPYA

Kwa tovuti yake mpya, muundo mpya, nembo mpya, na zana mpya za uendeshaji, BiVA hutoa fursa ya ufikiaji wa mamia ya maelfu ya vitabu, vitabu vya kiada, ensaiklopidia, makala na majarida katika nyanja zote za masomo, waelimishaji walisema.

 

“Uzinduzi huu unajumuisha matarajio ya jamii nzima yenye hamu ya kupokea nguvu ya elimu na maarifa,” mwenyekiti wa IAD Elie Henry alisema. “Maktaba ni nguzo na visima vya maarifa ambavyo vinatoa fursa zisizo na kikomo ili kwamba watu waweze kuchunguza, kugundua, na kukua. Hebu jukwaa hili muhimu lipatikane wakati wowote, liwe na manufaa, na kustawisha maisha ya watu wengi na jamii.”

 

 

NYENZO YA THAMANI

Mkurugenzi wa elimu wa IAD Faye Patterson alieleza shukrani zake kwa viongozi na wasimamizi wa IAD kwa kulipatia kanisa nyenzo hiyo muhimu sana.

 

“Katika ulimwengu unaobadilika kwa kasi, uwezo kwa ajili ya kuendelea kujifunza umegeuka kuwa uwezo muhimu, kugeuza maktaba za mtandaoni kuwa nguzo za msingi za mchakato wa elimu,” Patterson alisema. Shukrani kwa nyenzo mtandao, watoto na vijana katika maeneo ya mbali wanapata habari muhimu, alisema. “Kwa kuongeza, shule nyingi ambazo hazina maktaba halisia zinaweza kufanya utafiti, kutatua hitaji kubwa,” Patterson alisema.

 

Maktaba kubwa ya mtandaoni pia ni hitaji muhimu la uidhinishaji kwa taasisi za elimu katika ngazi zote, siyo tu kwa mfumo wa elimu ya Waadventista katika Divisheni ya Amerika, lakini pia kwa serikali katika kila nchi inayowakilishwa, alisema.

 

Divisheni ya Amerika ya Kusini inajumuisha mataifa 42 na maeneo ya visiwa kuanzia Mexico hadi Colombia na Caribbean kote.

 

 

MAENDELEO YA MAKTABA YA MTANDAONI

Maktaba hiyo ya mtandaoni imekuwa ikitoa nyenzo tangu mwaka 2007, lakini ilihitaji nguvu fulani kuboresha utendajikazi wake na kupanua rasilimali zake katika lugha ya Kiingereza, Kihispania, na Kifaransa, alisema Yanet Cima, mkurugenzi wa elimu msaidizi wa IAD. Cima, ambaye alipewa jukumu la kuongoza Maktaba Mtandao ya Waadventista ya mwaka 2021, alisema alifanya kazi bila kuchoka na timu ya watu stadi, wataalamu, na watu waliojitolea kutengeneza chapa upya, kupata moduli zilizo rahisi kutumia, kupanua rasilimali zake za ensaiklopidia na vitabu vya kiada, na kusimamia kila kitu kinachohusiana na usajili mpya wa maktaba ya mtandaoni.

 

“Inapendeza sana kuwa na maktaba hii ya mtandaoni karibu na shule zetu, ambayo inasaidia kuwahamasisha wanafunzi kusoma zaidi na kuchimba zaidi katika uchunguzi wao wa utafiti,” Cima alisema.

 

Mwaka 2023 zaidi ya kurasa milioni 3.3 katika BiVA zilisomwa, Cima aliripoti. Timu yake inatarajia kwamba idadi hiyo itaongezeka mwaka 2024. Maktaba ya mtandaoni huangazia nyenzo katika lugha ya Kihispania na Kiingereza na makala katika lugha ya Kifaransa, pamoja na chaguzi za tafsiri za Kifaransa.

Wachungaji kutoka madhehebu mbalimbali ya Kikristo hivi karibuni walifanya mkutano katika makao makuu ya Waadventista wa Sabato katika Jiji la San Pablo, Laguna, Ufilipino, kwa ajili ya Mradi wa PREACH (Project for Reaching Every Clergy at Home).

 

Idadi ya washiriki 56 kutoka katika majimbo ya Batangas, Laguna, na Quezon walihudhuria tukio hilo, lenye kauli mbiu “Feed My Lamb” (Lisha Kondoo Zangu). Lengo la msingi lilikuwa ni kubuni uhusiano chanya pamoja na wahudumu wengine wa kanisa na kushiriki umaizi wa kuhudumia vema mikusanyiko yao kwa kuelimisha welekevu wao, waandaaji walisema.

 

 

AFYA BORA KUPITIA KWA LISHE

Mawasilisho yaligusia maeneo mengi muhimu katika maisha na huduma ya wachungaji ikiwa ni pamoja na afya ya mwili na akili, muziki, familia, waumini na ukuaji binafsi wa kiroho. Watoa mada wote walitoka Union Konferensi ya Ufilipino Kaskazini (NPUC), ofisi kuu ya Kanisa la Waadventista wa Sabato huko Luzon.

 

Mkurugenzi wa huduma za afya wa NPUC, Jadaza Hintay, alizungumzia mada muhimu ya kudumisha afya ya mwili kupitia lishe sahihi, akielezea kuhusu viwango vya unene wa kupindukia na shinikizo la damu miongoni mwa wahudumu wa kanisa. Akisisitiza uhusiano kati ya lishe bora na ustawi wa kiakili, kijamii, kimwili na kiroho, Hintay alisisitiza umuhimu wa lishe kamili.

 

Baada ya hilo, mkurugenzi wa huduma za muziki wa NPUC, Josie-Felda Calera, alijadili umuhimu wa kulea roho kwa muziki, akielezea kama tulizo na kutia moyo, ikisaidia ustawi wa mwili na akili. Aidha, Ardie Diaz alifafanua umuhimu wa kuilisha akili chakula cha kiroho. “Kile unacholisha akili yako kitaamua afya ya hali yako ya kihisia na kiroho; itakumaliza au kukukamilisha. Kuilisha akili na ukweli wa Mungu kutakufanya uwe imara,” Diaz alisema.

 

Afisa wa faragha za data, Jose Orbe Jr., alielezea sababu tatu za kustawisha kanisa: kuimarisha upya, kusheheneza, na kuzalisha. Alisema, “Tukishindwa kuwaleta waumini kwa imani katika Mungu, wao ni wenye njaa. Wanaendelea kula lakini bado wanahisi njaa. Wanaendelea kunywa lakini bado wanahisi kiu. Tunapaswa kuwalisha nini? Kristo. Tutawalisha kwa namna gani? Kwa kuwaongoza kwa imani katika Kristo, Kristo atawatosheleza. Kristo anatosha.”

 

Katibu wa huduma wa NPUC, Marvin Diaz, alifunga kipindi na mada “Kumlisha Mchungaji kwa Lishe ya Kibiblia.” "Wakati kondoo wanapolishwa vizuri, maziwa ni mazuri,” Diaz alisema. Aliwahimiza wahudumu kuweka kipaumbele cha muda katika kusoma Neno la Mungu. “Furaha ya kweli huja tu kupitia Neno la Mungu. Neno la Mungu linatutakasa. Lazima tukutane na Neno la Mungu. Biblia si tu chombo kwa ajili ya kuhubiria; ni kwa ajili ya mabadiliko ya maisha yetu.”

 

 

MWITIKIO NA TAFAKARI

“Kila kitu hapa ni kitakatifu,” alisema Nestor P. de los Santos, mjumbe kutoka Kanisa la Jesus Christ Refiner’s Fire. “Tunaweza kuhisi uwepo wa Mungu. Tuna hamu ya kuiga utendaji wenu mzuri, mbinu na mafundisho na jinsi mnavyoishi kama Wakristo.”

 

Mchungaji mkuu Arcangel Santonia, wa Kanisa la The Light of the World, alitoa shukrani ya dhati kwa fursa ya kushiriki na wachungaji wa Waadventista. “Mkutano huu unaonyesha kuwa ingawa tunatoka katika mashirika tofauti, tunajumuika katika Roho mmoja na Mungu mmoja,” alisema.

 

Katika maelezo yake ya kufunga, Jasper Flores, mwenyekiti wa Konferensi ya Luzon, alitoa shukrani kwa wachungaji wote waliohudhuria. “Ni furaha kubwa kuwa na wachungaji wenzetu. Ni nia yetu kubadilishana uzoefu bora na kujifunza kutoka kwa kila mmoja ili kuimarisha huduma zetu,” Flores alisema.

Chini ya kauli mbiu yao “Every Ride a Mission” (Kila Safari ni Utume), washiriki 18 wa Huduma ya Pikipiki ya Waadventista (Adventist Motorcycle Ministry [AMM]) huko Ajentina walishiriki katika Mkusanyiko wa 10 wa Kimataifa wa Pikipiki wa Top of the World huko Uspallata, Mendoza, Februari 10-11.

 

Kikundi cha pikipiki cha Waadventista wa Sabato kiligawa asusa za kiafya na vitabu vyenye kuelimisha walipoungana na waendesha pikipiki wenzao waliofika kwenye sanamu ya Kristo Mkombozi ya Andes kwenye kivuko cha mpaka wa futi 12,572 kati ya Ajentina na Chile. “Lengo letu lilikuwa kumwonyesha Yesu katika mkusanyiko huo,” viongozi wa huduma walieleza.

 

Lengo hilo liliongoza kila kitu ambacho kikundi hicho kilifanya katika mkusanyiko katika Milima ya Andes. Lilihusisha kutoa kifungua kinywa cha bure kwa waendesha pikipiki kabla ya kuendesha kwenye kivuko cha mwinuko. “Pamoja na chakula, tulimpa kila mshiriki kitabu. Tuligawa vitabu vya Waadventista 3,000,” mwanachama wa AMM alisema. Kikundi pia kilitoa vinywaji na vitabu kwa waendesha pikipiki waliotoka upande wa Chile wa mlima.

 

“Tulijihisi kama askari 300 wa Gideoni,” mwanachama wa AMM alisema. “Tulikuwa 18 tukihudumia zaidi ya waendesha pikipiki 3,000, lakini kwa msaada wa Mungu, tulimhudumia kila mtu.”

 

Wanachama wa AMM Ajentina walisema kwamba hadithi moja ya Biblia iliwajia akilini, kuzidishiwa mikate na samaki na Yesu. “Shukrani kwa [kampuni ya Waadventista ya chakula cha kiafya] Granix, tulikuwa na biskuti za kugawa, lakini pia tuligawa tunda kama plamu, pichi na tikiti maji,” wanachama wa huduma walisema. “Wafadhili wenye ukarimu walitupatia matunda bure, ambapo inaonyesha jinsi Mungu anavyoingilia kati tunapomtafuta kwa mioyo yetu yote.”

 

 

KWENYE KAMBI LA WATAFUTANJIA

Siku chache baada ya tukio katika milima, wanachama wa AMM walihudhuria Kambi la Watafutanjia la Ajentina karibu na Rivadavia, Februari 14-18. “Tulipewa fursa ya kutambulisha na kushiriki kazi ya AMM hapo,” wanachama wa huduma hii walisema.

 

Mkusanyiko uliowaleta pamoja karibu Watafutanjia 8,000 kutoka nchi nzima ulikuwa kitovu cha sherehe iliyogusa hisia za watu, washiriki wa AMM walisema. Ismael, mwanachama wa AMM na baba wa mwanachama wa Klabu ya Watafutanjia, aliamua kutoa maisha yake kwa Mungu kupitia ubatizo. Ilishangaza, hata kwa familia yake.

 

Viongozi wa AMM walisema kwamba uongofu wa Ismael ulianza miezi kadhaa iliyopita. Wakati wa tukio la pikipiki la 2023 huko Mendoza, mratibu wa AMM Ajentina Néstor Espíndola alikwenda kumtembelea Ismael nyumbani kwake. “Ilikuwa wakati huo ambapo tulianza kuunda uhusiano, ambao ulipelekea masomo ya Biblia, na hatimaye uamuzi wa Ismael kubatizwa tena baada ya kuwa mbali na kanisa kwa muda,” Espíndola alisema.

 

Ismael alibatizwa na Pablo Geronazzo, mkurugenzi wa uinjilisti wa Union Konferensi ya Ajentina. Wakati wa tukio hilo, Geronazzo pia alisimikwa kuwa mwanachama mpya wa AMM Ajentina.

 

 

KUHUSU HUDUMA YA PIKIPIKI YA WAADVENTISTA

Wazo la “huduma kwa magurudumu” lilianzishwa Oktoba 2008 katika akili za Miguel Jesús Domínguez na wachungaji watano wa Waadventista huko Florida, Marekani, ambao, pamoja na watu wengine 60, walianzisha mpango huo. Kikundi hicho cha Wahispania kiliamua kwamba hakitakuwa tu klabu ya kawaida ya pikipiki, bali huduma, ili kufanya ufalme wa Mungu ujulikane kwa waendesha pikipiki wengine na kuwavuta watu kwa ajili ya mbinguni.

 

Juan Santos Siendo, mwenyekiti wa AMM USA wakati huo, alikuwa na jukumu la upanuzi wa huduma, kufikia sasa nchi nyingine kama Australia, Kanada, Hangari, India, Nepali, na Puerto Rico na baadhi ya nchi za Kiafrika. Huko Amerika Kusini, kuna vilabu rasmi vya AMM Ajentina, Bolivia, Brazili na Peru.

“Sidhani kama unaweza kulishinda hili.” Nilisema maneno hayo na kuyaacha yakining’inia hewani na kuangalia uso wa mwanafunzi kwa makini kuona angetoa jibu gani. Uso wake ulionyesha kushangazwa. “Unasema kuwa siwezi kufanya lolote kuhusu hili?” Nilitulia tena na kuchagua maneno yangu kwa uangalifu.

 

“Kwa kujitegemea mwenyewe, huwezi kusitisha. Wewe hujiwezi, lakini hujapoteza tumaini.” Nilirudi nyuma kwenye rafu yangu ya vitabu na kutoa nakala iliyochakaa ya Steps to Christ iliyoandikwa na Ellen White, nikifungua ukurasa wa 18. “Ni jambo lisilowezekana kwetu, wenyewe, kujinasua kutoka kwenye shimo la dhambi ambamo tumetumbukia. Mioyo yetu ni miovu, na hatuwezi kuibadilisha.”1

 

Inaweza kuonekana kuwa ni jambo la ajabu kuwaambia watu hawawezi kubadilika. Wengi wanataka ushauri, dawa, au mkakati. Kunaweza kuwa na thamani katika njia hizi. Lakini itakuwaje endapo tatizo, katika kiini chake, ni dhambi? Kitu wasichoweza kubadilisha. Basi, suluhisho linahitaji kitu zaidi cha msingi na cha maana. Linamhitaji Mwokozi.

 

 

HABARI MBAYA NA HABARI NJEMA

Moja ya vitabu vyangu ninavyopenda katika Biblia ni Warumi. Ni maelezo ya kuvutia sana ya injili ambayo nimeyapata. Lakini inashangaza jinsi Paulo anavyoanza hoja yake ya injili. Sura zake tatu za kwanza zinakamilika katika 3:23, “kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu.”

 

Hapa ndipo anapoanzia Paulo. Sisi ni wenye dhambi. Tunakaa katika uharibifu, tumejitenga na Mungu, wengine, na sisi wenyewe. Ni vigumu kwetu kukubali kuwa tatizo halisi ni dhambi, lakini kujua hali yetu kunatuwezesha kupokea dawa sahihi. Ikiwa mguu wangu ungevunjika, nisingetarajia daktari kuniambia niutembeze. Hapana, habari mbaya ya mguu wangu uliovunjika inanifanya nitazamie habari njema kwamba kuna daktari wa upasuaji ambaye anaweza kuirekebisha mifupa vizuri na kunielekeza kwenye njia ya uponyaji.

 

Katika kitabu chao cha kuvutia kuhusu How People Change, Timothy Lane na Paul Tripp wanatoa oni hili, “Ni pale tu unapoikubali habari mbaya ya injili ndipo habari njema inapoweza kuwa na maana. Neema, urejeshwaji, upatanisho, msamaha, rehema, subira, nguvu, uponyaji na tumaini la injili ni kwa ajili ya wenye dhambi. Ni vya maana kwako tu ikiwa unakiri kuwa una ugonjwa na kugundua kuwa ni wa hatari.”2

 

 

MBINU ZISIZOFAA KWA DHAMBI

Mara tu tunapogundua kuwa tatizo halisi ni dhambi, lazima tukubali suluhisho la Mungu kwa hiyo. Cha kusikitisha, hata Wakristo wanashughulikia dhambi kwa njia zisizofaa. Mbinu ya kwanza isiyofaa kwa dhambi ni ya kutojali. Inatokana na mtazamo wa Mungu, ambao unamwona akitoa msamaha bila kuhitaji mabadiliko kabisa au utii. Dietrich Bonhoeffer, mwandishi wa Kitabu cha The Cost of Discipleship, akiita hii kuwa “neema rahisi.” Ni “neema” ambayo tunajipa sisi wenyewe na hivyo ni neema bila Yesu.3

 

Mtu asiye na haja ya mabadiliko hatafanya mabadiliko. Hawatafikia ushindi kwa sababu hawaoni haja ya kuona kuwa unahitajika au hata unaweza kufikiwa. Huu ni mtazamo wa uongo wa injili kwa sababu unaona Mungu akishughulikia dhambi bila kubadilisha mkosaji.

Mbinu nyingine isiyofaa kwa dhambi ni aibu. Inajengwa juu ya wazo kwamba tunapaswa kuwa na aibu kwa tuliyoyafanya tunapokosea. Kadiri tunavyoona aibu zaidi, ndivyo tunavyokuwa “wenye kufanya toba” zaidi. Aibu ni tofauti na hatia kwa sababu wakati hatia inatufanya tukimbilie Mwokozi, aibu inatuondoa kwa Mungu na kuingia kwenye hisia zetu wenyewe. Adamu alihisi aibu katika Bustani ya Edeni, badala ya hatia, na kukimbia kutoka kwa Mungu.

Aibu ni njia isiyofaa sana ya kukabiliana na dhambi kwa sababu ni aina ya kujikomboa. “Ikiwa ninaweza kujihisi vibaya vya kutosha, basi kwa namna fulani itafuta dhambi yangu.” Hii inatufanya tufanye dhambi zaidi kwa sababu tunaweza kujishughulikia kupitia hisia zetu mbaya. “Ikiwa nimekosea, nitajihisi vibaya baadaye, na kisha niweze kuendelea na maisha yangu.”

 

Mbinu ya mwisho isiyofaa kwa dhambi ni kutumia mikakati ambayo itajaribu kudhibiti au kusimamia tabia zetu. Lakini hii pia haifai. Tabia ni tunda tu la mzizi mrefu. Kuweka vichujio kwenye kompyuta haitabadilisha hamu ya ponografia. Hatimaye, mtu aliye na azimio atapata njia katika vichujio. Tatizo halisi ni moyo na tamaa zake (Yakobo 1:14-15). Isipokuwa tubadilishe tamaa zetu, tabia hizo zitaendelea kujirudia.

 

Basi, tunawezaje kubadilisha moyo? Steps to Christ inaelezea tatizo na suluhisho. “Huwezi kulipia kosa kwa ajili ya dhambi zako za zamani; huwezi kubadilisha moyo wako na kujifanya kuwa mtakatifu. Lakini Mungu anaahidi kufanya haya yote kwa ajili yako kupitia Kristo.”4 Hili linaturudisha tena kwenye injili katika kitabu cha Warumi.

 

 

SULUHISHO NI NEEMA

Baada ya Paulo kutuambia kuwa sote tunateseka kwa athari mbaya za dhambi, anatambua suluhisho. “Tukiisha kuhesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu” (Warumi 3:24). Suluhisho la tatizo la dhambi ni Mwokozi.

 

Kuna maneno matatu muhimu katika aya hii. La kwanza ni “kustahili bure.” Inavuta picha ya mtu anayesimama mbele ya jaji ambaye anatangaza kuwa “hana hatia.” Hukumu hii kwa urahisi inatoka kwa Mungu, ambaye, badala ya kumweka mkosaji katika hukumu ya haki, anamwacha kuwa huru. Lakini mtu mwenye hatia anawezaje kutangazwa kuwa asiye na hatia?

 

Jibu lipo katika aya inayofuata, ambayo inatamka kuwa hii hufanyika “kwa neema Yake.” Neema inamhusu Mungu kuonyesha fadhila kwa watu ambao hawastahili. Kwa kuwa dhambi zetu hatimaye ni kinyume na Mungu, Yeye pekee ndiye anayeweza kuzisamehe. Ingawa sisi ni wenye hatia, Mungu anatoa msamaha Wake kwa hiari. Hata hivyo, hii sio neema duni (isiyo na thamani).

 

Billy Graham anatoa mfano wa hili. Alikamatwa akipita kasi katika mji mmoja wa kusini na kwenda mahakamani. Jaji aliamua kuwa alikuwa na hatia, na faini ilikuwa dola 10, dola 1 kwa kila maili zaidi ya kikomo cha kasi. Ilikuwa kitu ambacho kilipaswa kulipwa. Lakini, jaji alimtambua mwinjilisti maarufu, akachukua dola 10 kutoka mfukoni mwake mwenyewe kulipa faini, na kumkaribisha Graham kujiunga naye kwa chakula cha jioni!5 Neema ilikuwa ya bure, lakini bado ilihitaji malipo.

 

Kirai cha mwisho katika aya hii kinaeleza kuwa neema hii hufanyika “kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu.” Ukombozi una maana ya uhuru ulionunuliwa kwa bei. Ikiwa mtu alifanywa mtumwa kwa sababu ya deni, wangeweza kuachiliwa huru kwa fidia - mtu fulani analipa madeni yao. Yesu alilipa deni hilo kwa ajili yetu.

 

Basi, hili linawezaje kumsaidia mtu anayepambana na tabia za uraibu? Badala ya kuzingatia dhambi, tunapaswa kumzingatia Mwokozi. Yesu tayari amelipa bei. Tayari amenunua uhuru wetu. Tunapaswa kuishi katika mwanga wa ukweli huo, na kisha uhuru ulionunuliwa tayari unakuwa wetu.

 

 

KWA NINI TUNAHITAJI MWOKOZI

Tukimtazama Yesu, tunagundua anatupatia masuluhisho matatu yenye nguvu dhidi ya dhambi. Kwanza kabisa, Yesu alifuta fidia ya dhambi. Biblia inasema “mshahara wa dhambi ni mauti” (Warumi 6:23), na Yesu alijitokeza na kulipa hiyo kwa ajili yako.

 

“Aliwafanya hai pamoja naye, akiisha kutusamehe makosa yote; akiisha kuifuta ile hati iliyoandikwa ya kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu; akaiondoa isiwepo tena, akaigongomea msalabani.” (Wakolosai 2:13-14).

 

Pili, Yesu alitoa pigo la kifo kwa utawala wa dhambi na nguvu yake katika maisha yako. Paulo anasema dhambi “haitawatawala ninyi” (Warumi 6:14). Hii haimaanishi kuwa tamaa zako za dhambi zimepotea. Inamaanisha kuwa nguvu mpya sasa inafanya kazi. Msalaba ulionyesha kuwa Yesu alifanikiwa pale ambapo Adamu alishindwa. Tamaa za binadamu zilishindwa, na dhambi sasa ilikuwa adui aliyeshindwa.

Hata hivyo, Yesu si Mwokozi wetu tu kwa sababu alikufa kwa ajili yetu, bali pia kwa sababu anaishi kwa ajili yetu, akiomba kwa niaba yetu. “Kwa kuwa hamna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi. Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji” (Waebrania 4:15-16).6 Tunapata ushindi juu ya dhambi kwa sababu Yesu anatupa neema na nguvu tunayoihitaji tunapopata majaribu.

 

Tatu, Yesu alikuja kama Mwokozi wetu ili kwamba uwepo wa dhambi uweze kutokomezwa kutoka ulimwenguni. Mapambano na dhambi hayataendelea milele. Amani yetu ya baadaye imehakikishiwa. Kila wakati tunapopata ushindi juu ya dhambi, tunashiriki katika ukweli wa baadaye wa ulimwengu kamili ambapo upendo hutawala sana na ubinafsi kuondolewa.

 

Tunapojua kuna mwisho, tunaweza kuegemea katika kuumaliza mwendo kwa nguvu.

Hii ndiyo habari ya injili. Neno “injili” lina maana ya habari njema. Ni habari njema kwamba tatizo ni dhambi kwa sababu basi suluhisho ni Mwokozi. Ni habari njema kwamba fidia ya dhambi imeondolewa kwa wote wanaomwamini Kristo. Ni habari njema kwamba nguvu ile ile iliyompa Yesu ushindi ndiyo inapatikana kwako sasa. Ni habari njema kwamba Yesu ni Mwokozi wako mbinguni sasa, akiomba kwa niaba yako. Ni habari njema kwamba hukumu inakuja ambayo itaondoa dhambi milele kutoka ulimwenguni.

HAKI KWA IMANI

Hii inatuleta kwenye jambo la mwisho kuhusu suluhisho la Mungu. Mabadiliko huja kupitia imani. Imani haipo katika wewe mwenyewe, bali imani katika Mwokozi wako. Imani si tu kuamini bali ni uchaguzi. Ni kumtegemea Mungu na kujitoa maisha yako Kwake.

 

“Kristo hubadilisha moyo. Anakaa moyoni mwako kwa Imani. Unapaswa kudumisha uhusiano huu na Kristo kwa Imani na kuendelea kuisalimisha dhamira yako Kwake, na kadiri utakavyofanya hivi, atafanya kazi ndani yako kufanya kulingana na ridhaa Yake nzuri.”7 (tazama pia Wafilipi 2:12-13).

 

Haki kwa imani ndivyo jinsi Mungu anavyotubadilisha. Hatutegemei neema isiyo na thamani kuondoa hitaji la utii. Hatujichukii wenyewe au kutumia mikakati kufanya mabadiliko yatokee. Tunamgeukia Yesu. Tunamtazama Yeye. Tunaweka imani yetu Kwake na kuchagua njia ya kujisalimisha badala ya njia ya kujitegemea.

 

Nilipokuwa kijana, nilikwenda baharini kwa mara ya kwanza. Nilijua kuogelea, lakini sikuzoea mawimbi ya bahari. Kabla sijajua, nilinaswa na mawimbi ya mkondo na nilikuwa nikivutwa mbali na pwani. Nilijaribu kuogelea kurudi pwani, lakini haikusaidia. Kwa bahati nzuri, mwokozi aliniona na kuja kunisaidia. Nilijaribu kumwambia kuwa nitakuwa sawa, lakini yeye alijua vizuri. Aliniambia nisiogelee tena na nimwamini. Alinichukua na kuniweka kwenye boti yake ya uokoaji kwa mikono yake yenye nguvu na kunivuta salama kurudi pwani. Bila msaada wake, ningezama majini siku ile, kwa kutegemea uwezo wangu wa kujiokoa mwenyewe.

 

Haki kwa imani ni kumtumaini Yesu atuokoe na kisha kumchagua Yeye na kujisalimisha kwake kila siku. Hii haitakuwa rahisi. Kuna siku ambazo dhambi zako zitapata ushindi. Kutakuwa na siku utakazojihisi mbali na Mungu. Lakini katika siku hizo, kumbuka msemo ule wa zamani, “Kwa vyovyote vile, bado Yesu ni Mwokozi wangu.” Badala ya kujilinganisha, mwangalie Yesu. Endelea kumwangalia “tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu” (Waebrania 12:2).

 

 

BADO YESU NI MWOKOZI WANGU

Kulitokea nini kwa mwanafunzi yule aliyejikuta akisumbuliwa na dhambi ya uraibu? Alikata tamaa ya kujaribu kuitatua mwenyewe. Siku ile, alisalimisha maisha yake kwa Yesu. Hakukuwa na suluhisho la haraka, lakini kadiri alivyomtazama Yesu zaidi, ndivyo moyo wake ulivyobadilika. Badala ya kutegemea hisia zake, alimtegemea Mwokozi wake. Na jinsi moyo wake ulivyobadilika, ndivyo tamaa zake zilivyobadilika. Alimpenda Yesu. Alijifunza kwamba licha ya chochote alichokumbana nacho, “bado Yesu  ni Mwokozi wangu.” Na msifu Mungu, alipata ushindi!

Makala hii msingi wake ni katika hubiri katika Kanisa la Waadventista wa Sabato la Living Hope mnamo Septemba 13, 2019. Vipengele vya uwasilishaji wa mdomo vimehifadhiwa.—Wahariri.

 

 

John Wesley, mhubiri maarufu wa Methodist, alikuwa karibu na kukata tamaa. Hakuwa na imani ya kuendelea kuhubiri. Alikuwa amechoka na afya yake ilikuwa inazorota. Wakati kifo kilimkabili, alikuwa na hofu na hakupata faraja kubwa katika dini yake. Alifunua siri kwa rafiki yake kwamba alikuwa tayari kuacha huduma ya kuhubiri. Mnamo Mei 24, 1738, alifungua Biblia yake saa kumi na moja asubuhi na akakutana na maneno haya katika 2 Petro 1:4 “Tena kwa hayo ametukirimia ahadi kubwa mno, za thamani, ili kwamba kwa hizo mpate kuwa washirika wa tabia ya Uungu.” Je, Umewahi kugundua kwamba wakati wa huzuni kubwa au majaribu makali zaidi, Mungu hukuelekeza katika aya sahihi ya Biblia unayoihitaji wakati huo ili kukutia moyo? Matumaini yalianza kudhihirika moyoni mwa Wesley.

 

Jioni hiyo alihudhuria mkutano kwa shingo upande katika Kanisa la Aldersgate huko London. Mtu fulani alisoma kutoka kwa dibaji maarufu ya Luther Utangulizi kwa kitabu cha Warumi. John Wesley alikaa katika kanisa hilo la kawaida usiku huo akisikiliza kwa makini. Baadaye aliandika maneno haya katika jarida lake. “Takribani saa 2:45 usiku, wakati Luther alipokuwa akielezea mabadiliko ambayo Mungu anayafanya moyoni kwa imani katika Kristo, nilihisi moyo wangu kupatwa na joto la ajabu. Nilihisi nilimwamini Kristo, Kristo pekee kwa wokovu; na nilihakikishiwa kwamba alikuwa ameniondolea dhambi zangu, hata zangu, na kuniokoa kutoka katika sheria ya dhambi na kifo.”1

 

Hebu tuchunguze katika barua ya Paulo kwa Warumi kile inachofundisha kuhusu maisha ya Kikristo ya ushindi.

 

 

UNATEMBEAJE?

Warumi 8:1 inatuambia “Sasa, basi, hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu.” Neno hukumu ya adhabu linamaanisha hukumu dhidi ya mtu ikiwa ni pamoja na fidia inayofuatana na hukumu hiyo. Paulo anachosema ni kwamba katika Kristo tumekombolewa kutoka katika utaratibu wa zamani wa utumwa, hukumu na utumwa katika maisha mapya ya msamaha, nguvu na uhuru. Kisha anaendelea kuelezea njia mbili za maisha: Maisha katika mwili na maisha katika Roho.

 

Paulo anamaanisha nini kwa kusema, “kutembea katika mwili?” Paulo hana maana ya mwili tu wa nyama kwa maana ya mwili, kama tunavyosema “mwili na damu.” Kwa kweli humaanisha asili ya binadamu katika udhaifu wake wote na udhaifu wa dhambi. Kuishi kulingana na mwili wa nyama ni kuishi maisha yanayodhibitiwa na amri na tamaa za asili ya dhambi ya binadamu badala ya maisha yanayodhibitiwa na amri na upendo wa Mungu. Mwili wa nyama ni upande dhaifu wa asili ya mwanadamu. Unahusiana na mielekeo, hisia kali, misukumo, na hamu ya tamaa zetu za mwili, dhambi na asili ya ubinafsi.

 

Kinyume chake, Paulo anasisitiza kutembea kulingana na Roho. Paulo anasema katika aya hii kwamba kulikuwa na wakati ambapo Mkristo alikuwa katika rehema ya asili yao wenyewe ya dhambi, hisia kali na matamanio yao wenyewe, uchu na tamaa zao wenyewe. Katika hali hiyo, sheria ikawa kitu ambacho kiliwasukuma kufanya dhambi na kutoka pabaya hadi pabaya zaidi, mtu aliyeshindwa na kukata tamaa. Lakini kwa karama ya Mungu, uweza mkuu wa Roho wa Mungu uliingia katika maisha yao, na, kama matokeo, wakaingia katika maisha ya ushindi.

 

 

UGUNDUZI WA AJABU

Paulo anaendelea kutofautisha kati ya sheria mbili zinazofanya kazi: Sheria ya Roho wa uzima ule ulio katika Kristo Yesu na sheria ya dhambi na mauti (Rum. 8:2). Sheria hii ya dhambi na mauti ni nini? Jibu linapatikana katika Warumi 7. Paulo anaelewa kwamba sheria ni takatifu, ya haki na njema (Warumi 7:12) lakini kuna mapambano halisi yanayoendelea maishani mwake. Aliamua kufuata sheria hii ya Mungu lakini kwa haraka aligundua kwamba pamoja na sheria hii nje yake, kulikuwa na sheria nyingine ndani yake moja kwa moja inayopingana na sheria nje yake (aya ya 23). Wakati sheria ya Mungu nje yake iliposema, “utafanya jambo hili jema na hili jema na hili jema,” sheria ya urithi au asili yake iliyopotoka ndani yake ilisema “huwezi kufanya jambo unalotaka.”

 

Sheria ya asili iliyopotoka inashinda, na majaribio ya Paulo kuishi maisha ya haki huishia kufeli kabisa. Kulingana na Warumi 7 anajikuta akizama zaidi na zaidi katika matope ya dhambi, akishurutishwa na kuvutwa chini na sheria hii ya dhambi mpaka hatimaye anapiga kelele katika Warumi 7:24, “Ole wangu, maskini mimi! Ni nani atakayeniokoa na mwili huu wa mauti?”

 

Inavutia kwamba kiwakilishi “mimi” kinaonekana mara 27 katika aya kumi na tano katika Warumi 7:9-24, na Roho Mtakatifu hapatikani hata mara moja. Katika sura ya 8 ya Warumi, hali inabadilika kwa kiasi kikubwa na Roho Mtakatifu anatajwa mara 20 wakati “mimi” inatajwa mara mbili tu.

 

Katika Warumi 8 Paulo anafunua ugunduzi wa ajabu. Mbali na sheria ya Mungu nje yake ikimhimiza kwa haki na sheria ya viungo vyake au sheria ya urithi katika asili yake iliyopotoka, kuna sheria nyingine! Ni “sheria ya Roho wa uzima katika Kristo Yesu” (Warumi 8:2). Sheria hii ni juu ya haki ambayo huwezi kuifikia kwa uwezo wako kwa nguvu ya mapenzi yako mwenyewe. Hatuwezi kufikia haki ambayo sheria inadai kwa nguvu zetu wenyewe, kwa sababu ya udhaifu wa asili yetu iliyopotoka. Hivyo, Warumi 8:3.

 

Hakuna shida kwenye sheria. Kama Paulo anavyosema katika Warumi 7, ni takatifu, ya haki na njema. Shida haiko kwenye sheria. Ipo kwangu. Nikiwa peke yangu sina uwezo kabisa wa kukidhi mahitaji ya sheria. Mimi ni mdeni wa sheria ambayo nimeivunja, nimehukumiwa kwa makosa yangu, na kuwekwa utumwani kwa asili yangu ya dhambi. Lakini kisha Yesu akaja na kukutana na Shetani mahali ambapo wanadamu wote wameanguka, katika udhaifu wa mwili wa binadamu.2 Yesu aliingia uwanjani kwa masuala ya kibinadamu kupigana vita pamoja na wanadamu wote. Aliichukua asili yetu ili kujifungamanisha pamoja nasi na kuja kumshinda Shetani (tazama Ebr. 2:14-18).

 

 

HITAJI LETU KUBWA ZAIDI

Kama vile msemo huu unaohusishwa na Roy Lessin unavyosema:

“Ikiwa hitaji letu kuu lingekuwa habari, Mungu angetutumia mwalimu.

Ikiwa hitaji letu kuu lingekuwa teknolojia, Mungu angetutumia mwanasayansi.

 

Ikiwa hitaji letu kuu lingekuwa fedha, Mungu angetutumia mchumi.

Ikiwa hitaji letu kuu lingekuwa raha, Mungu angetutumia msanii.

Lakini hitaji letu kuu lilikuwa uhuru kutoka katika fidia na nguvu ya dhambi, kwa hivyo Mungu alitutumia Mwokozi.”

 

Tukifikia mwisho wetu, tunapotambua kabisa uwezo wetu wa kuishika sheria ya Mungu na katika udhaifu kamili kumtazama Kristo na kumtegemea Roho Mtakatifu kutenda kwa ajili yetu yale ambayo hatuwezi kufanya kwa ajili yetu wenyewe, na tunaposalimisha kila wazo na kila kusudi na kila tamaa, kila kitendo na uchu wote na hamu zetu kwa udhibiti wake kamili, Roho Mtakatifu anachukua udhibiti wa maisha yetu na kutuweka huru kutoka katika nguvu ya dhambi inayokaa katika asili yetu, na kutuleta katika ulinganifu na mapenzi ya Mungu (tazama Warumi 8:4).

 

Ikiwa tunapigana kwa nguvu zetu wenyewe, tunapigana vita vinavyoshindwa, lakini katika Kristo sisi ni zaidi ya washindi (Wagalatia 5:16, 17). Hii ni moja ya sababu ya ugumu wa kushinda tabia za mtindo wa maisha ambazo tunajua zinatuangamiza. Hii ndiyo sababu ni vigumu kushinda hisia na tamaa zetu. Hii ndiyo sababu ni vigumu kushinda tabia zisizo za Kikristo. Hii ndiyo sababu tunapambana kwa kweli kuwa watu tunaotaka kuwa na kufanya mambo tunayotaka kufanya. Ikiwa tunapigana na adui kwa nguvu zetu wenyewe, tutashindwa kila wakati.

 

Hakuna sababu ya kuendelea kuwa utumwani tena. Yesu anapokaa ndani yetu, tunawekwa huru kutoka katika udhalimu na utawala wa asili yetu ya dhambi. Chini ya utaratibu wa zamani haiwezekani kufanya mapenzi ya Mungu. Tunaweza kujua kilicho sahihi, lakini hatuna uwezo wa kufanya hivyo. Tunaweza kutamani kufanya jambo sahihi lakini mara kwa mara tunashindwa kwa sababu sisi ni wadhaifu sana kufikia tamaa zetu. Tunaweza hata kutaka kushinda tabia zisizo njema na mtazamo hasi lakini tunarudi nyuma kwa mazoea hayo ya zamani tena na tena.

 

Warumi 8 inaleta mfumo mpya kabisa. Kwa Paulo, maisha ya Kikristo si tena ya kushindwa kwa kufadhaika. Si tena ya utumwa na utawala. Roho Mtakatifu anayejaza maisha ya muumini ametuweka huru. Warumi 8 ni mahali pa kwanza katika kitabu cha Warumi ambapo Roho Mtakatifu anaingia katika mjadala, na anapofanya hivyo, hakuna mazungumzo zaidi ya kushindwa. Vita kati ya asili hizo mbili bado vinaendelea, lakini ambapo Roho Mtakatifu anadhibiti, asili ya zamani inalazimika kutoa njia. Kuishi katika nguvu za Roho Mtakatifu haina maana kwamba tutakuwa huru kutoka katika mapambano. Inamaanisha kwamba tuna uhakika wa ushindi katika mapambano yetu. Inamaanisha kwamba Kristo amepeana nguvu za kushinda kila jaribu kupitia kwa Roho Mtakatifu kukaa ndani yetu (tazama kwa mfano 1 Kor. 10:13).

 

Hii hapa ahadi ya Mungu: “Nami nitawapa ninyi moyo mpya, nami nitatia roho mpya ndani yenu, nami nitatoa moyo wa jiwe uliomo ndani ya mwili wenu, nami nitawapa moyo wa nyama. Nami nitatia roho yangu ndani yenu, na kuwaendesha katika sheria zangu, nanyi mtazishika hukumu zangu, na kuzitenda” (Ezekieli 36:26).

UWEZA WA ROHO

Roho ni mwenye nguvu. Anaweza kubadilisha moyo wa jiwe kuwa moyo wa nyama; anaweza kubadili tabia mbaya zaidi kama ngome ya mchanga ikivunjika mbele ya mawimbi; anaweza kufanya mambo magumu zaidi kuonekana rahisi, na pingamizi kali zaidi kuyeyuka kama theluji wakati wa majira ya joto; anaweza kuvunja minyororo, kufungua milango ya gereza na kufungua milango ya ushindi; anaweza kujaza kila bonde na kufanya kila mahali palipokwaruzwa kuwa pazuri. Amefanya hivyo mara nyingi, na anaweza kufanya tena.

 

Uweza wa Roho Mtakatifu hauna kikomo. Uweza wa Roho Mtakatifu si kwa watakatifu wachache waliochaguliwa. Uweza wa Roho Mtakatifu sio wa karne ya kwanza kwa kanisa la awali. Roho Mtakatifu ni kama Bwana Yesu, yule yule jana, leo na hata milele. Yeye bado anaendelea kufanya miujiza na ataendelea kufanya hivyo hadi mwisho.

 

Yesu alishinda mamlaka na nguvu za kuzimu. Alikuwa mshindi ili tuweze kuwa washindi kupitia Roho Wake kwa nguvu Yake. Maana ya kutembea katika Roho ni nini? Kutembea katika Roho ni neno ambalo mtume Paulo alilitumia mara kwa mara kuelezea kuishi katika uwepo wa Kristo kupitia Roho Mtakatifu. Ni utambuzi wa kila siku kwamba mimi ni Wake na Yeye ni wangu. Ni ile njaa ya kila siku ya kumjua zaidi. Ni kugundua furaha ya kumimina mioyo yetu kila siku kwa Mungu.

 

Miaka kadhaa iliyopita, kijiji kidogo Afrika kilipitia uamsho wa nguvu wa Roho Mtakatifu. Wengi katika kijiji hicho walibadilishwa na nguvu ya Roho Mtakatifu. Tamaa ilipisha usafi. Kujijali mwenyewe kulipisha kujisalimisha. Wizi ulipisha uaminifu. Hasira ilijisalimisha kwa wema na ulafi kwa kutoa.

 

Kila mmoja wa waongofu hawa wa Kiafrika inasemekana alikuwa na mahali katika kichaka ambapo walikuwa wakimimina mioyo yao kwa Mungu kila siku. Njia kupitia kwenye nyasi ndefu ili kuelekea mahali hapa pa maombi zilifahamika. Wakati mtu yeyote alipoanza kurudi nyuma katika maombi yake, ilikuwa wazi kwa wengine. Kisha wangemkumbusha kwa kusema, “Ndugu, nyasi zinakua katika njia yako kule.” Je, nyasi zinakua katika njia yako? Tukitembea katika mwili tutashindwa kila wakati. Kutembea katika Roho, kuishi katika mwanga wa uwepo wa Kristo, sisi ni zaidi ya washindi. Mtume anahitimisha Warumi 8 kwa maneno haya yenye tumaini katika Warumi 8:37: “Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda.” Haya ni maneno yenye tumaini. Yanatupa ujasiri wa kukabiliana na changamoto za maisha.

 

Hatujakusudiwa kushindwa. Ushindi ni wetu katika Kristo kupitia nguvu ya Roho Mtakatifu.

Kwa Paulo, maisha hayakuwa yenye kuchosha, kutarajia kushindwa; yalikuwa yenye nguvu, yenye matarajio dhahiri. Mkristo anashiriki katika hali ya kibinadamu. Ndani yake lazima apigane na asili yake mwenyewe ya dhambi; nje lazima aishi katika ulimwengu wa mauti na uharibifu. Walakini, Mkristo haishi tu katika ulimwengu; pia huishi ndani ya Kristo. Hauoni tu ulimwengu; hutazama ng’ambo ya pili kwa Mungu. Hayaoni tu matokeo ya dhambi ya wanadamu; huona nguvu ya huruma na upendo wa Mungu. Kwa hivyo, kauli mbiu ya maisha ya Kikristo, daima ni tumaini na kamwe usikate tamaa. Mkristo hungojea, si mauti, bali uzima.

Tukio muhimu katika historia ya vuguvugu la Marejeo ni Sikitiko Kuu la Oktoba 22, 1844, waumini walipotarajia Ujio wa Bwana na walivunjika moyo sana wakati hakurudi. Ingawa wengi walikata tamaa, kundi dogo lilishikamana na Neno la Mungu. Walisoma na kuomba hadi walipogundua kwamba ufunguo wa kufumbua siri ya kuvunjika moyo kwao ulikuwa katika kuelewa kile Biblia inafundisha kuhusu patakatifu.1

 

Huu ulikuwa ni ufunuo mkuu sana kwa waumini Waadventista wa kwanza kwa sababu, kama vile Ellen White anavyoeleza, “Ulifungua mfumo kamili wa ukweli, ulioshikamana na kuafikiana, ukionyesha kuwa mkono wa Mungu uliongoza vuguvugu kuu la marejeo na ulifunua wajibu wa sasa kwa kuonyesha nafasi na kazi ya watu Wake.”2

 

Waumini Waadventista wa kwanza walipojifunza, uzuri na umoja wa Maandiko ulianza kung’aa ndani ya mioyo na akili zao. Waliona uhusiano wa unabii katika Danieli 8:14, “Hata nyakati za jioni na asubuhi elfu mbili na mia tatu; ndipo patakatifu patakapotakaswa,” na tangazo la malaika wa kwanza wa Ufunuo 14, “Mcheni Mungu, na kumtukuza, kwa maana saa ya hukumu yake imekuja” (aya ya 7).

 

Walielewa vizuri kwamba “Kristo alikuwa amekuja, sio duniani, kama walivyotarajia, lakini, kama ilivyokuwa imetabiriwa katika mifano, ndani ya patakatifu pa patakatifu katika hekalu la Mungu mbinguni.”3

 

Tukio hili lilielezewa na nabii Danieli: “Nikaona katika njozi za usiku, na tazama, mmoja aliye mfano wa mwanadamu akaja pamoja na mawingu ya mbingu akamkaribia huyo mzee wa siku, wakamleta karibu naye” (Dan. 7:13).

 

Waligundua kuwa nabii Malaki alikuwa anaelezea tukio hilo hilo alipoandika, “Bwana mnayemtafuta atalijilia hekalu lake ghafula; naam, yule mjumbe wa agano mnayemfurahia, angalieni, anakuja, asema Bwana wa majeshi” (Mal. 3:1).

 

“Kuingia kwa Bwana katika hekalu Lake” kulikuwa kwa ghafla, bila kutarajia, kwa watu Wake, kwa sababu hawakumtarajia kwenda pale. Walimtarajia kuja duniani!

 

 

KAZI YA MAANDALIZI

Zaidi ya hayo, hawakuwa tayari bado kumpokea Bwana wao. Tunaambiwa “bado kulikuwa na kazi ya maandalizi kwa ajili yao.”4

 

Aya ya Malaki 3:2, 3 inaelezea wazi kazi hii:

“Lakini ni nani atakayestahimili siku ya kuja kwake? Au ni nani atakayesimama atakapoonekana yeye? Kwa maana yeye ni mfano wa moto wa mtu asafishaye fedha, ni mfano wa sabuni ya mtu afuaye nguo; naye ataketi kama asafishaye fedha na kuitakasa, naye atawatakasa wana wa Lawi, atawasafisha kama dhahabu na fedha; nao watamtolea Bwana dhabihu katika haki.”

 

Akiifafanua aya hii ya Malaki, mjumbe wa Bwana aliandika:

“Watakaokuwa wakiishi duniani wakati maombezi ya Kristo yatakoma katika hekalu la mbinguni watasimama mbele ya macho ya Mungu bila mpatanishi. Majoho yao yanapaswa yasiwe na doa, tabia zao zinapaswa ziwe zimesafishwa kutoka dhambini kwa kunyunyiziwa damu ya Yesu Kristo. Kwa njia ya neema ya Mungu na kwa njia ya juhudi binafsi inawapasa wawe washindi katika vita dhidi ya uovu. Wakati hukumu ya upepelezi ikiendelea mbinguni, wakati dhambi za waaminio wanaotubu zikiondolewa hekaluni, kuna kazi maalum ya utakaso ambayo inapaswa ifanywe, ya kuachana na dhambi, miongoni mwa watu wa Mungu duniani. Kazi hii imewasilishwa kwa uwazi zaidi katika ujumbe wenye sehemu tatu wa Ufunuo 14. Wakati kazi hii itakapokuwa imekamilika, wafuasi wa Kristo watakuwa tayari kwa ajili ya ujio Wake. . . . Ndipo kanisa ambalo Bwana wetu wakati wa ujio Wake atalipokea litakuwa “Kanisa tukufu, lisilo na ila wala kunyanzi wala lolote kama hayo.’ ”5

 

 

KAZI MAALUM YA MUNGU

Kwa mara ya kwanza, hii inaweza kuonekana kama jambo lenye kugharikisha. Lakini tusipoteze lengo kwamba hii ni kazi maalum ya Mungu ya utakaso! Yeye ndiye anayetoa “vazi lisilo na waa.” Ni damu Yake inayotutakasa. Ni neema Yake inayotupa nguvu ya “kuwa washindi katika vita dhidi ya uovu.” Mungu pekee Ndiye anayeweza kutusaidia kuwa washindi katika vita dhidi ya uovu—bila Yeye tu wapotevu bila tumaini katika dhambi.

 

Wakati wa hekalu la duniani, Siku ya Upatanisho ndiyo iliyokuwa siku muhimu zaidi ya mwaka. Watu walitafakari mioyo yao, walitubu dhambi zao na kuhakikisha walikuwa katika upatanifu na Mungu. Kwa kuwa sasa tunaishi katika “kipindi cha hukumu ya upelelezi,”6 aya hii inatukumbusha kwamba Mungu anatamani kutakasa mioyo yetu na kutuandaa kama watu binafsi na kama kanisa, kwa ujio Wake ulio karibu.

 

 

MATUKIO MAWILI TOFAUTI

Wakati baadhi wanaweza kuamini aya hii katika Malaki 3 kurejelea Ujio wa Kristo wa mara ya pili, Ellen White anaweka bayana kwamba ingawa Malaki anazungumzia ujio wa pili katika baadhi ya aya, hii siyo mojawapo. Anaandika: “Ujio huu, na kuja kwa Bwana ndani ya hekalu Lake, ni matukio mawili yaliyo tofauti kabisa.”7

 

Anaelezea zaidi, “Kuja kwa Kristo kama kuhani wetu mkuu ndani ya patakatifu pa patakatifu, kwa ajili ya utakaso wa hekalu, kunakotajwa katika Danieli 8:14; kuja kwa Mwana wa Adamu kwa Mzee wa Siku, kama kulivyoelezwa katika Danieli 7:13; na kuingia kwa Bwana ndani ya Hekalu Lake, kulikotabiriwa na Malaki, ni maelezo ya tukio lile lile moja.”8

 

Kwa uwazi, Biblia inasema kwa sauti moja inapotangaza kipindi cha hukumu ya upelelezi—wakati tunaoishi sasa.

VAZI LA ARUSI

Katika Mathayo 22, Yesu anazungumza juu ya karamu ya arusi. Katika mfano huu, uchunguzi wa hukumu unafanyika wakati mfalme anachunguza wageni ili kuhakikisha wote wamevaa vazi la arusi alilotoa kwa upendo. Vazi hili la tabia lisilo na mawaa, linalowakilishwa na vazi la arusi, limeoshwa na kufanywa jeupe kwa damu ya Mwana-Kondoo, kama ilivyoelezwa katika Ufunuo 7:14.

 

Katika mfano huo, mfalme anamkaribia mmoja wa wageni ambaye hakuvaa vazi la arusi na kumuuliza kwa upole, “Rafiki, uliingiaje humu nawe huna vazi la arusi?” (Mt. 22:12). Mgeni huyo hakusema neno.

 

“Mfalme akawaambia watumishi, Mfungeni mikono na miguu, mchukueni mkamtupe katika giza la nje; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno” (aya ya 13).

 

Rafiki, je, umevaa vazi la haki la Kristo? Je, unamruhusu akusafishe katika damu ya Mwana-Kondoo? Sasa ni wakati wa kumruhusu afanye kazi Yake maalum ya utakaso mioyoni mwetu ili tuwe tayari kwa Ujio Wake.

Taarifa zinatoka katika baadhi ya nchi kwamba wanawake hawaruhusiwi kuzungumza kwenye mimbari katika baadhi ya makanisa ya Waadventista wa Sabato wakati wa siku zao za hedhi. Kitendo hiki kinategemea dhana mbili. Kwanza, inaonekana kwamba mahali ambapo mimbari ipo ndani ya kanisa ina utakatifu kama ule wa patakatifu pa kale pa Israeli, ambapo palilazimika kulindwa kutokana na unajisi wa ibada ya kimwili. Pili, inaonekana kwamba sheria za kibiblia kuhusu unajisi wa ibada ya kimwili bado zinatumika leo. Kulingana na Walawi 15:19-23, mwanamke wa Israeli wakati wa kawaida wa hedhi yake alipata unajisi wa ibada ya kimwili ambao ungeweza kuenezwa kwa vitu na watu kwa kugusana. Baadhi wanachukulia hii kuwa inamaanisha kuwa Biblia inakataza mwanamke Mwadventista wa kisasa kusimama kwenye mimbari wakati anapokuwa katika hedhi.

 

 

MATOKEO YA DHANA MBILI

Ikiwa tungekubali dhana hizi mbili, tungepaswa kufuata kwa uadilifu sheria zote za usafi za kibiblia, sivyo? Kwa hivyo, kwa mfano, ikiwa tutatumia Hesabu 19:14 leo hii, yeyote ambaye amekuwa chini ya paa moja na mtu mfu, ikiwa ni pamoja na kuwa kwenye mazishi, angekuwa najisi. Kulikuwa na njia moja tu kwa Mwisraeli kujitakasa kutoa unajisi wa maiti: kunyunyiziwa maji maalum yaliyo na majivu ya ng’ombe (chakula) mwekundu ambaye alitolewa kafara kwa njia iliyoelezwa na Mungu kwa ushiriki wa kuhani wa ukoo wa Aruni (Hesabu 19:1-10, 12, 17-19, 21).1

 

Ni Waadventista wangapi wamenyunyiziwa maji ya utakaso yaliyo na majivu ya ng’ombe mwekundu? Hakuna, kwa sababu hiyo haiwezekani leo. Kwa hivyo, Waadventista wote ambao wamekuwa najisi kutoka kwa maiti wanabaki najisi milele.

 

Ili kukubaliana, ikiwa wanawake wanazuiwa kuzungumza kanisani wakati wa hedhi zao, hakuna mtu yeyote ambaye amehudhuria mazishi, ikiwa ni pamoja na mchungaji (ambaye huenda amehudhuria mazishi zaidi kuliko mtu mwingine yeyote!), angepaswa kuruhusiwa kuzungumza pia. Hii haiwezekani, na kuna sababu rahisi: tutagundua kuwa dhana zote mbili ni za kubuni.

 

 

UTAKATIFU WA KANISA LA KIKRISTO?

Makanisa yetu ya Kikristo si patakatifu kama patakatifu pa kale pa Israeli, ambapo palikuwa patakatifu kwa sababu ya Uwepo wa Mungu, ambao ukifunikwa na wingu la utukufu lililoonekana, uliwepo huko duniani miongoni mwa watu Wake (Kut. 25:8; 40:34-38; Walawi 16:2). Makanisa yetu hufanya kazi kama sinagogi katika wakati wa Yesu, ambapo watu wa kawaida wangefika kwa heshima kusikiliza Neno la Mungu likisomwa na kufafanuliwa (Luka 4:16-27). Lakini watu wasiokuwa makuhani walizuiwa kuingia patakatifu pa Israeli au hekalu baadaye (Hes. 3:38; 18:7).

 

Kwa sababu makanisa yetu si mahali patakatifu kama patakatifu pa Israeli, unajisi wa kimwili wa ibada hauwezi kuathiri sehemu yake yoyote. Wala hakuna tofauti yoyote ya utakatifu katika makanisa yetu kana kwamba eneo la jukwaa linalingana kwa njia fulani na mahali patakatifu au patakatifu zaidi pa patakatifu pa Israeli.

 

 

MATUMIZI YA SASA YA SHERIA ZA UNAJISI?

Sheria za Agano la Kale kuhusu unajisi wa ibada ya kimwili zinatufundisha kuhusu asili ya Mungu katika uhusiano wetu, lakini hahitaji tuzitumie leo hii.2 Unajisi kama huo ulitokana na maiti za binadamu (Hes. 19), mtiririko kutoka katika viungo vya uzazi vya binadamu (Walawi 12, 15), na maambukizi mabaya katika ngozi ya binadamu, kitambaa au ngozi, au kwenye kuta za nyumba (Walawi 13-14), pamoja na baadhi ya aina za maiti za wanyama (Walawi 11:24-40).3 “Unajisi” wao haukuwa uchafu halisi, na maambukizi kutoka kwao, yaliyonajisi vitu vingine kwa kugusana au ukaribu, hayakuwa ya kimwili. Badala yake, unajisi wa kimwili wa ibada uliwakilisha mzunguko wa kuzaliwa-hadi-kufa kwa mwanadamu anayepatikana na mauti uliotokana na dhambi (Mwa. 3; Rum. 6:23),4 ambapo maiti, mtiririko kutoka katika viungo vya uzazi, vyenye afya au ugonjwa, n.k., ni dalili. Ni kweli kwamba mtiririko wa usiku, kujamiiana, hedhi, na kujifungua ni kufanya kazi vizuri kwa mifumo ya uzazi ya binadamu, lakini unajisi kutoka kwa hivi unafundisha kwamba kila mtoto anayezaliwa katika ulimwengu wetu uliopotoka hataishi milele, hufa.

 

Mungu ni Mtakatifu, asiye na dhambi, Safi, Chanzo cha uzima wote, na hatahusishwa na mauti au dhambi ambayo imeyasababisha. Kwa hivyo, sheria Zake za kuzuia unajisi wa kimwili wa ibada ikiwezekana au kuziponya (kwa kunawa, kusubiri hadi jioni, na pia kafara katika masuala muhimu) zilikuwa na lengo la kuwafundisha watu Wake kumhusu Yeye na kuhusu dhambi na mauti ambayo imewatenga Naye. Kafara ya Kristo, iliyowakilishwa kwa kafara za Israeli ambazo ziliponya si dhambi tu (kwa mfano, 4:1-6:6), bali pia unajisi mkubwa wa kimwili wa ibada (Walawi 12:6-8; 14:10-32; 15:14-15, 29-30; Hes. 19:1-10), hutuokoa si tu kutoka kwa matendo yetu ya dhambi ili kutupa msamaha, bali pia kutoka katika hali yetu ya mauti ili kutupa uzima wa milele (Yn. 3:16).5

 

Tunaweza kujifunza mengi kwa kusoma sheria za unajisi wa ibada za kibiblia ambazo zilikuwa lazima kwa Waisraeli wa kale, lakini Mungu hatahitaji tuzitumie. Sasa Kristo anahudumu kama kuhani wetu mkuu katika hekalu la Mungu mbinguni (Ebr. 4:14-16; 6:19-10:25), ambalo halina uchafu wa kibinadamu. Kwa hivyo, mfumo wa kanuni za kulinda hekalu la kidunia kutokana na unajisi haufai tena. Wengi wetu ni najisi kulingana na sheria katika vitabu vya Walawi na Hesabu, lakini hii haina maana! Agano Jipya halisemi chochote kuhusu mahitaji ya utakaso wa kimwili wa ibada kwa yeyote ili kushiriki katika jukumu lolote la kanisa.

DHANA KAMA VISASILI VISIVYO VYA KIBIBLIA

Tumegundua kwamba dhana mbili zinazounga mkono kitendo cha kukataza wanawake kuzungumza mimbarini wakati wa hedhi zao ni visasili visivyo vya kibiblia. Kwa hivyo, kitendo hiki si cha kibiblia. Kushikilia sana kanuni kama hizo ambazo zilikuwa sehemu ya mfumo wa “vivuli” vya ibada ambavyo viliashiria ujio wa Kristo (linganisha na Kol. 2:17) vinamwakilisha Mungu visivyo kwa kutokubali kwamba Kristo amekuja kweli na amehamishia mahali pa huduma Yake kwenye hekalu la mbinguni la Mungu.

 

Sera zetu za kanisa zinapaswa kuundwa kwa nuru ya ufunuo kamili wa Maandiko kwa ujumla, badala ya kuchagua kile tunachokiona katika Biblia. Kuhusu wanawake kuzungumza katika makanisa ya Waadventista, wanapaswa kuwa huru kuzungumza wakati wowote bila kuulizwa maswali binafsi yasiyofaa.

Mwaka 1977, dada yangu alirudi nyumbani mwishoni mwa juma moja kutoka chuo cha Avondale akiwa na marafiki wawili kutoka California. Tulikuwa tukiishi katika eneo la Mashariki zaidi huko Australia, Pwani ya Wategos, Ghuba ya Byron. Nyumbani kwetu kulikuwa na mandhari ya kupendeza ya bahari, tambarare za pwani na milima ya mbali ya Mpaka na safu za milima za kupendeza. Mlima mkubwa uliokuwa umbali wa maili 27.5 ulikuwa ni Mlima Wollumbin, kama ulivyopewa jina awali la asili la Bundjalung na taifa. Kilele chake cha itale kilifanana na mwamba uliolala wenye nundu. Mwaka 1770, mgunduzi Mwingereza Kapteni James Cook aliuita, Mlima Warning.

 

Rafiki zetu wapya, waliovutiwa na mlima huo, waliuliza ikiwa wangeweza kuupanda. “Bila shaka!” Baba alishangilia, daima akiwa tayari kwa uvumbuzi. Kwa hivyo, tukiwa watu saba tukaanza safari kwa gari katika mandhari nzuri ya Jumamosi mchana kuelekea Hifadhi ya Taifa ya Wollumbin. Tulipofika ilikoanzia njia, tulichukua miongozo kadhaa kabla ya kuelekea kwenye njia yenye kona nyingi ya maili 5.5.

 

Kwanza, tulizunguka kupitia misitu ya mitende yenye mvua ya Bangalow na miti ya mtini ya Ghuba ya Moreton. Mara, njia ikawa na changamoto, ilikuwa na miinuko mirefu na mikali na majabali mengi yaliyo hatari. Baada ya kupanda kwa muda mrefu, hatimaye tulitoka kwenye msitu wenye mvua na kufika kwenye ukingo wa mlima. Hatua ya mwisho ya Mlima Warning ni kupanda kufikia kilele chake cha futi 3,800.

 

Tulifikia kilele cha mlima kwa wakati ili kushuhudia jua la Sabato likizama, likitupatia miali mirefu ya mwanga kote chini. Baada ya kutazama mandhari, Baba alituhamasisha kuondoka, lakini rafiki zetu Wamarekani waliduwaa, wakivutiwa na mandhari ya kushangaza iliyozunguka kilele cha mazingira ya volkano ya kale. Tulimaliza Sabato wakati miali ya mwisho ya jua ilipoisha juu ya upeo wa macho, tukiomba kwa ajili ya usalama wa kushuka.

 

 

HATARI KUBWA GIZANI

Tukiwa na nguvu mpya, tuliiteremka kwa kasi njia yenye mchanga na utelezi, tukifika kwenye njia ya changarawe giza lilipofunika. Kwa haraka tulitembea kwenye njia nyembamba, lakini tulifanikiwa kupitia vilima viwili tu kabla ya kugubikwa na usiku. Usiku usio na mwezi uliongeza hali yetu ngumu. Tukijikwaa tulipotembea gizani, akili zetu zilianza kufikiria kuhusu hadithi za wapanda milima waliopotea kwa siku kadhaa, mara nyingine milele, mlimani.

 

Ghafla, nilisikia kilio cha Baba na wito wa mbali wa msaada. Alikuwa ameanguka futi kumi chini ya ukingo, akigonga mti uliomshikilia asitokomee zaidi. Baada ya kumsaidia, maombi ya shukrani kwa Mungu yalitolewa. Baba yangu sasa alitumia fimbo ya kutembelea kwa uangalifu kufuatilia njia yake. Polepole, kundi letu lilishuka mlimani, tukiweka mguu mmoja imara dhidi ya ukingo wake. Kile kilichokuwa furaha saa mbili hapo kabla sasa kilikuwa jinamizi; tulijuta kutozingatia saa za matembezi zilizowekwa za Mlima Warning.

 

Tulikuwa tumetoka nyumbani bila tochi. Tukiwa hatujajiandaa kwa giza la usiku, tulijikwaa katika msitu wa mchikichi wa Bangalow. Hapa, tulikutana na wapanda milima wawili waliopotea. Tukiunganisha juhudi, tulichana ramani zetu za hifadhi katika vikaratasi vyembamba na kutumia kiberiti chao kuziteketeza. Mwale wa vimetameta ulitoa mwanga wa kutosha kuongoza njia yetu, hadi tulipofika kwenye msitu wa mvua nzito karibu na msingi wa mlima. Hapa, kwa majuto, karatasi zetu zilikwisha. Tukipambana, mara tukapotea kabisa. Bila mahali pengine pa kugeukia isipokuwa maombi, tulimwomba Mungu kwa ajili ya msaada.

 

Kwa kweli, baada ya muda mfupi tu, yadi 200 kutoka mlimani, mwanga mkali ulionekana. Tukisikia sauti nyingi za furaha, tulijua maombi yetu yalikuwa yamejibiwa! Klabu ya Watafutanjia ya Murwillumbah ilionekana na kutuongoza kwenye eneo la maegesho! Walikuwa njiani kuelekea mlimani kupiga kambi na kutazama jua likichomoza. Saa nne za kuhuzunisha baadaye, safari yetu ya kushuka Mlima Warning ilikuwa imekwisha. Tulimsifu Mungu kwa wema Wake na huruma kwa kutuma “Klabu ya Watafutanjia ya Waadventista” kutuokoa!

KUSONGA MBELE

Hadithi hii inanikumbusha ibada ya Ijumaa jioni. Baba yangu alisoma kuhusu maono ya kwanza ya Ellen Harmon. Akiwa amezingirwa na nuru, Ellen aliinuka juu na juu kutoka duniani ambapo alishuhudia watu wanaosubiri Ujio wakipita njia nyembamba kwenda mbinguni. Nuru kubwa iliangaza nyuma yao, ikiwazuia wasijikwae njiani. Ikiwa wangeendelea kukaza macho yao kwa Yesu, ambaye aliwaongoza kuelekea Jiji Takatifu, wangekuwa salama. Lakini baadhi yao walichoka, wakilalamika kuwa jiji lilikuwa mbali sana. Walitarajia kuwa tayari wangekwisha kuliingia. Yesu aliwahimiza, akiunyosha mkono Wake wa kuume ulioangaza kwa utukufu, ukimulika njia kwa ajili ya kundi la wasafiri waliosubiri Ujio. Baadhi yao kwa upumbavu waliikana nuru hii, hata hivyo, wakisema kwamba Mungu hakuwa akiwaongoza. Kwa wale wenye dhana hizo, nuru ilizimika. Wakiwa wamepofushwa kwa giza, walijikwaa kwenye lindi kuu. Cha kusikitisha, wakishindwa kumwona Yesu, walipotea milele kwenye ulimwengu wenye dhambi.1

 

Kwa mawazo yangu, hadithi zote zinaonyesha haja yetu ya kuwa tayari. Wazazi wangu walionyesha matayarisho haya. Walitumia muda kila siku katika sala, kusoma Neno la Mungu na kusoma kutoka katika Roho ya Unabii. Tangu nikiwa mdogo, nilijifunza umuhimu wa sala na ibada ya familia. Binafsi, nilishuhudia Neno la Mungu kama “taa kwa hatua zangu na mwanga kwa njia yangu” (Zaburi 119:105). Kumbuka, “tunapaswa kujiandaa kwa maisha na tabia ili kukabiliana na mahitaji ya nyakati zilizo mbele yetu.” Kama watu waaminifu wa Mungu, lazima tujitayarishe kwa ajili ya Ujio wa Yesu.

 

Kama Waadventista, je, bado tunaamini sehemu ya pili ya jina letu? Tunaamini katika Sabato, lakini je, tunaishi kama kurudi kwa Yesu kunakaribia? Tunakiri kuwa Wakristo wenye kusoma Biblia, lakini je, tunasoma Neno la Mungu kila siku? Je, tunasoma mara kwa mara kutoka katika Roho ya Unabii? Au tumeshaanguka kwenye shimo la usingizi wetu wa Laodikia, tukipotea katika vishawishi vya ulimwengu wenye dhambi?

 

Lazima tuamke! Hatuwezi kuanguka gizani ikiwa tutamfanya Kristo kuwa kiongozi wetu. Yesu anasema, “Anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima” (Yohana 8:12). Hii ndiyo sababu, “njia inapoonekana kuwa ngumu na kufunikwa na giza, lazima tuamini kwamba kuna nuru mbele yetu na tusigeuke kulia au kushoto, bali tusonge mbele, licha ya majaribu yetu yote na majaribio.”3

 

Mungu amelibariki kanisa Lake kwa karama ya unabii. Maandishi ya Ellen White yanatuelekeza daima kwenye Neno la Mungu kama chanzo halisi cha nuru. Vitabu vyake vinasisitiza umuhimu wa kutii Maandiko na kujiandaa sisi wenyewe na wengine kwa ujio wa pili wa Kristo.4 Hakuna mtu atakayejikwaa na kuanguka ikiwa atazingatia maonyo dhahiri—kama tulivyopaswa kufanya kabla ya kupanda Mlima Warning. Wakati wa kujiandaa ni sasa! Kesho haina hakikisho. Mbingu haiwezi kuja hivi karibuni zaidi! Je, uko tayari?

Miaka 20 iliyopita, washiriki wa kanisa mahalia la Waadventista walijisikia kutakiwa na Mungu kuanzisha kanisa. Wakaanza kujenga mahusiano na watoto na familia kule Hannover, wilaya mpya kabisa nchini Ujerumani  kupitia kushiriki katika elimu ya kivitendo.  Mnara mrefu wa kukwea (“Life Tower”) punde ukawa nembo maarufu kwa maeneo ya ujirani. Kupitia ujenzi wa mahusiano ya kijamii yenye ufanisi, programu ile ikatambuliwa kama sauti muhimu katika ujenzi wa mahusiano ya kijamii katika wilaya hiyo.

 

Huduma ya Life Tower bado ni programu inayoendelea, lakini bado haijaweza kuanzisha kanisa la Waadventista. Je, huku ni kushindwa?

Mmoja wa wanachama waanzilishi wa awali kabisa anaieleza hivi: “Tulikuwa na njozi, ndoto, na malengo yetu. Kadiri miaka ilivyopita, tulishuhudia kufaulu na kushindwa. Ilibidi tukubali kuwa watu tunaowahudumia wanaweza kuhitaji kitu tofauti na tulichokusudia. Je, tuwaangushe kwa sababu tu hawaitikii jinsi tunavyotaka? Kama tungefanya hivyo ingeonyesha kuwa haikuwa kwa manufaa yao, bali yetu. Badala yake, tuliamua kuendelea kutembea katika njia ya Kristo.”

 

Hivyo programu hii imepanuka na kujumuisha mchungaji, mtumishi wa ustawi wa jamii, na viongozi wengi wanaojitolea kutoka kwa makanisa mawili mahalia, washirika wetu wa huduma zingine, na wanajumuia. Programu ya Life Tower Kronsberg imebadilishwa kutokea kuwa programu ya kujitegemea hadi kuwa mtandao changamani ambapo maisha yanakuwa bora kuliko yalivyowahi kuwa. Sisi ni wajumbe wa kudumu wa baraza la huduma kwa vijana la wilaya, mara nyingi tukishirikiana kuongoza miradi (programu) za pamoja. Kanisa la Waadventista wa Sabato linaendelea kutambuliwa na kupata hadhi njema jijini.

 

 

CHANGAMOTO

Kila programu ya kuanzisha kanisa hupata changamoto—kijamii, kifedha, au hata changamoto za ndani. Kitu chochote kipya kinachoanzishwa katika ujirani hutazamwa kwa wasiwasi. Kwa jamii ya Kijerumani isiyo ya kidini, miradi yenye mazingira ya kidini, hupata ugumu kupata sifa njema. Mara nyingi watu huchukulia kuwa huduma za kijamii zaweza kutumika katika uongoaji wa roho, au hata kibaya zaidi kwa ajili ya kutia kasumba. Sisi binafsi tumesikia juu ya hofu za jinsi hii.

 

Vipi kama tukizuia ari ya kujihami,  na badala yake tumakinike katika utume wetu huku tukiwa na imani katika kanuni za kinabii? Vipi kama kwa dhati tukiutakia amani na ustawi mji ule tunaouhudumia? Vipi kama kwa moyo wote tukiuombea mji ule, kwa maana kama ukistawi, sisi pia tutastawi (Yer. 29:7)?

 

Jamii inayotuzunguka inajumuisha jamii mchanganyiko – watu kutoka utaifa, tamaduni, rangi, mazingira ya kidini yanayotofautiana kabisa. Kadiri, iwezekanavyo tunazingatia muktadha huo na kuhubiri “injili ya milele,” habari njema ambayo inatakiwa kuhubiriwa kwa kila “taifa, kabila, lugha na jamaa” (Ufu. 14:6).

Watu na familia nyingi ambazo zinashiriki katika shughuli zetu zinapata mazingira salama pasipo na vurugu wala ubaguzi wanapoweza kushiriki na kukua. Kupata mafanikio haya halikuwa jambo rahisi, lakini Mungu hajawahi kutuangusha.

 

 

MBINU YA KRISTO

Ellen White anatoa mashauri haya yanayofahamika sana kwa wote wanaoshiriki katika utume: “Ni mbinu ya Kristo pekee itakayoleta mafanikio ya kweli katika kuwafikia watu. Mwokozi alichangamana na watu kama aliyeyaonea shauku mema yao. Alionyesha huruma Yake kwao, aliyahudumia mahitaji yao na kusababisha wawe na Imani Naye. Kisha akawaagiza, ‘Nifuateni.’ ”

 

Anaelezea hatua tano, ambazo hakuna hata moja inayopaswa kurukwa. Kama tukiwaharakisha watu, jitihada zetu zaweza kukwama. Nyakati zingine, katika ari yetu ya kimishenari tunaharakisha mno kuelekea katika hatua ya mwisho. Vipi kama kufikia hatua ya mwisho kutachukua muda zaidi kuliko ambavyo tungependa kukiri? Je, tunaweza kupitia hatua za awali kwa subira? Kama tukijiondoa kwenye jamii, basi njia ya Yesu haikufanana na mipango mikakati kwa ajili ya mafanikio yetu.

 

 

VIKWAZO

Life Tower imekuwa sehemu ya maisha ya ujirani na inatimiza kusudi lake kama moja ya wakala wenye ufanisi mkubwa kabisa katika huduma kwa vijana na familia. Tumepata msaada kutoka Konferensi ya Hanseatic, Unioni ya Ujerumani Kaskazini, Divisheni ya Ulaya-Kati,  na kutoka Konferensi Kuu hasa kutoa fedha kwa ajili ya raslimali watu. Uwekezaji mahususi, kama vile urejeshaji wa mnara wa kukwea, zimefadhiliwa kifedha na washirika wetu wa nje wenye njozi na dhamira kama yetu.

 

Moja ya vikwazo vikubwa kabisa ambavyo programu hii imekabiliana navyo imekuwa suala la malipo kwa ajili ya ardhi tuliyokodisha. Mwezi Januari 2024 tulipokea baruapepe kutoka katika jiji la Hannover, ikisema: “Tunachukulia kuwa, ninyi, pia mngependa kubadilisha mkataba wenu wa muda kuwa wa kudumu.” Maneno, “Ninyi, pia” yalijaza mioyo yetu kwa furaha, kwa vile utawala wa jiji ulituonyesha kuwa sisi ni mshirika anayetumainika na kuhitajika katika wilaya hii. Mvuto wetu na thamani yetu inayotambulika katika wilaya ya Kronsberg vilidhihirika katika mkataba mpya na wa kudumu. Kwa eneo letu lenye ukubwa meta za mraba 4,200 tunalipia pango la ardhi la yuro 21 (takribani dola 23 za Marekani) kwa mwezi, ni kama kadirio la gharama ya chakula katika mkahawa.  Mkataba wetu mpya unaonyesha ushirikiano mwema wa kusaidiana kwa manufaa yetu na ya watu tunaowahudumia.

 

 

NJOZI ILIYOHUISHWA

Mnamo mwaka 2021 tulifanya upya njozi yetu, maadili yetu ya msingi, na maeneo yetu ya mkazo kwa msaada wa Taasisi ya Tathmini ya Friedensau (FIFE). Mchakato huu ulikuwa ushirikiano wa mwaka mmoja ambapo vipengele vyote vya dhamira yetu vilijadiliwa na Waadventista, watu wa jamii mahalia, na washirika tunaoshirikiana nao ili kujenga msingi ambao utalisaidia kanisa na wilaya.

 

Malengo haya mapya yalisababisha kuanzishwa kwa huduma ya utafutaji huria hewani katika Life Tower, kama njia mpya ya kushuhudia na kuchunguza njia ambazo kwazo kazi ya Mungu katika jamii tayari imejidhihirisha yenyewe. Muda unaonekana kuwa mwafaka kuunganisha sasa na lengo la msingi la kuanzisha kanisa.  Na hivyo mwezi Novemba 2023, tulianzisha ushirikiano na Taasisi ya Utume ya Arthur Daniells (ADIMIS), iliyopo katika Chuo Kikuu cha Waadventista cha  Friedensau, ili kupata mafunzo. Tunahitaji kupima upya uelewa wetu wa maana hasa ya “kuanzisha kanisa” hasa katika mazingira haya. Programu ya Life Tower ya Kronsberg yawezekana isibadilishwe kuwa kanisa la kawaida, lakini tuko wazi na wenye furaha kujua kuwa Mungu anaweza kutumia programu hii kufanya hata kitu kikubwa zaidi.

 

Bila shaka tunaweza kuona kwa kutazama nyuma kuwa kisa halisi hakikuwa kanisa kuanzisha kanisa bali kanisa kuanzisha mradi kuijenga jamii (kujenga mahusiano ya kijamii) kazi ambayo kwa yenyewe imezaa kanisa jipya.

Paulo hatoi aya ya Biblia aliyoitumia. Kwa kweli, katika mazungumzo ya Agano Jipya kuhusu kufufuka kwa Yesu katika siku ya tatu, hatupati rejea dhahiri kutoka katika aya ya Biblia. Tutafanya muhtasari wa matumizi ya neno “siku ya tatu” katika Agano Jipya, baadhi ya majibu yaliyotolewa kwa swali lako na kupendekeza jibu yumkini.

 

 

“KATIKA SIKU YA TATU.”

Kauli hii inapatikana kikamilifu takribani katika Injili, hasa kinywani mwa Yesu. Angekuwa “siku tatu mchana na usiku katika moyo wa nchi (Mt. 12:40); Atakufa na “siku ya tatu kufufuka” (Mt. 16:21; 17:23; Luka 9:22); “siku ya tatu atafufuka” (Mt. 20:19); “siku ya tatu atafufuka” (Luka 18:33; 24:7). Viongozi Wayahudi walijua kuhusu unabii wa Yesu kwamba “baada ya siku tatu nitafufuka” (Mathayo 27:63). Yesu aliposema, “Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na kufufuka siku ya tatu” (Luka 24:46), alikuwa akitangaza kwamba kufufuka Kwake siku ya tatu kulikuwa utimizwaji wa unabii. Ni dhahiri kuwa utimizwaji wa unabii huo katika siku ya tatu kulingana na Maandiko ulikuwa ndicho kiini katika ujumbe Wake.

 

 

MAJIBU YALIYOPENDEKEZWA:

Baadhi wamependekeza kwamba katika 1 Wakorintho 15:4 kauli “kama yanenavyo Maandiko” inatumika tu kwa kufufuka na si kwa “siku ya tatu.” Hili linawezekana lakini halielezi Luka 24:46. Uchunguzi wa aya umewaongoza wengine kutambua Hosea 6:2 kama unabii wa kufufuka siku ya tatu (“siku ya tatu atatuinua”) ambao sasa unatumika kwa Yesu. Hili linawezekana, lakini aya hii haihusiani waziwazi na kufufuka kwa Yesu katika Agano Jipya. Yona 1:17 pia imetajwa hasa kwa kuwa inarejelewa na Yesu katika uhusiano wa kauli “siku tatu” (Mt. 12:40). Wengine wameona kwamba aya nyingi katika Agano la Kale zinataja matukio muhimu ya ukombozi yakitokea siku ya tatu (k.m., Mwanzo 22:4 [kutoka kifoni siku ya tatu]; Kutoka 19:16 [kukutana na Mungu siku ya tatu]; 2 Wafalme 20:5-6 [mfalme kama aina ya Kristo]; Hosea 6:2). Wamehitimisha kwamba aya hizi kwa pamoja zina unabii unaoashiria kufufuka kwa Yesu kama tukio kuu la ukombozi wa Mungu katika siku ya tatu. Huu ni uwezekano mwingine mzuri. Hatimaye, kuna pendekezo kwamba kutoa malimbuko katika siku ya tatu baada ya kutoa dhabihu ya mwana-kondoo wa Pasaka (Walawi 23:11) kulionyesha kielelezo cha kufufuka kwa Kristo katika siku ya tatu. Kwa bahati mbaya, siku ya tatu haijatajwa waziwazi katika aya hiyo ingawa inaeleweka waziwazi.

 

 

UAMUZI MGUMU

Majadiliano yaliyopita yanatuonyesha kwamba hatuwezi kuwa na hakika katika kuchagua aya fulani kuwa unabii maalum wa kufufuka kwa Kristo katika siku ya tatu. Nitatambulisha kile ninachoona kuwa chaguzi mbili zilizo bora zaidi. Uchaguzi wa kwanza ni Yona 1:17. Kwa nini? Kulingana na Yesu, tukio la siku tatu la Yona katika eneo la kifo lilikuwa ishara, kama unabii wa kielelezo, wa kufufuka Kwake katika siku ya tatu (Mathayo 12:40). Hili, likiungana na kielelezo cha kutoa malimbuko siku tatu baada ya kafara ya Pasaka, kuwakilisha kufufuka kwa Yesu baada ya kujitoa Kwake mwenyewe kafara siku ya Pasaka, hutoa unabii madhubuti kwa kufufuka kwa Yesu katika siku ya tatu.

Tumeumbwa kwa jinsi ya ajabu ya kutisha. Hedhi ni namna muhimu ya kila mwezi inayoimarisha sehemu muhimu sana ya afya ya uzazi wa mwanamke, na kuakisi  zawadi ya ajabu iliyoundwa na Mungu na kuaminiwa na Mungu ya uzazi wa binadamu. Kuelewa undani wa hedhi ni muhimu, si tu ili kukuza ustawi wa wanawake, bali pia kwa kuvunja unyanyapaa wa kijamii unaouzunguka mzunguko huu wa asili.

 

Kuvunja ungo, kunaashiria mwanzo wa mchakato huu wakati wa kubalehe na hukoma katika umri wa makamo. Mzunguko wa hedhi ni mchanganyiko wa mabadiliko ya homoni unaoundwa na hypothalamus, teziubongo na ovari. Kwa wastani, huchukua siku 28, ukigawanywa katika awamu tofauti ziitwazo hedhi, folikali, kupevuka kwa yai na kukuza. Hedhi yenyewe ni kumwaga kwa utando wa mfuko wa uzazi ikiwa mimba haijatokea. Mchakato huu wa mzunguko una mabadiliko ya homoni, haswa estrogeni na progesterone, ambayo inadhibiti ukuaji na upevushaji wa yai (ovum) na kuandaa mfuko wa uzazi kudumisha uwezekano wa mimba.

 

Wakati hedhi ni muhimu kibiolojia, jamii ulimwenguni kote zimeendelea kudumisha miiko ya utamaduni na fedheha juu ya hilo. Dhana hizi za kijamii zinachangia kudhalilisha wanawake, kukuza mazingira ya aibu na ukimya. Elimu imechukua jukumu muhimu katika kufuta fedheha ya hedhi. Kutekeleza mipango kamili ya elimu ya ngono ambayo inajumuisha habari juu ya hedhi, msingi wake wa kifiziolojia, na kawaida yake kunaweza kukabiliana na dhana potofu na kuboresha uelewa.

 

Kushiriki katika mazungumzo ya hadhara kuhusu hedhi husaidia kuondoa uongo na kuongeza msaada wa kijamii. Kufanya mazungumzo ya kawaida kuhusu hedhi katika shule, maeneo ya kazi na katika kaya hupunguza fedheha inayohusiana. Vyama vya kitamaduni na dini vinaweza kukuza zaidi mtazamo chanya kuhusu hedhi kwa kufuta habari potofu inayoendeleza aibu.

 

Nchi zinazoendelea zinakabiliwa na upatikanaji mdogo wa vifaa vya usafi kwa wasichana wadogo. Ukosefu huu wa usafi sahihi wakati wa hedhi unaweza kusababisha masuala ya afya na kuathiri vibaya elimu ya msichana kupitia siku alizozipoteza kwa kutokwenda shuleni. Jamii lazima ziipatie kipaumbele mipango ya kutoa bidhaa za usafi zinazofaa kwa gharama nafuu na endelevu kwa mazingira kama vile vijikombe vya hedhi vinavyoweza kutumika tena na taulo za kike za kitambaa.

 

Mipango ya elimu shuleni inapaswa kutoa habari juu ya mazoea sahihi ya usafi na matumizi ya vifaa hivi vya usafi. Serikali na asasi zisizo za serikali wanaweza kushirikiana katika kutekeleza sera na mipango ambayo inahakikisha usambazaji wa bidhaa za hedhi, bure au zenye ruzuku katika shule na jamii. Kwa kuongezea, mipango inayohimiza kuanzishwa kwa miundombinu sahihi ya usafi, ikiwa ni pamoja na vyoo safi na binafsi, na upatikanaji wa maji safi, unaweza kuchangia sana katika kudumisha usafi wa hedhi. Shirika la Maendeleo na Utoaji wa Msaada la Waadventista (Adventist Development and Relief Agency [ADRA]) linashirikiana kwa dhati katika malengo haya.

 

Kama kanisa, Waadventista wa Sabato wanahimiza afya na ukamilifu kwa wote. Afya ya wanawake isiachwe nyuma. Jumuisha wanaume na wavulana katika mazungumzo. Elimisha kupitia makanisa yetu, shule, na taasisi za huduma za afya. Kwa kushughulikia unyanyapaa/fedheha ya kijamii na kutoa vifaa vya usafi kwa ajili ya vijana katika nchi zinazoendelea, tunaweza kukuza jamii ambayo inadidimiza fedheha ya hedhi, na kila mwanamke na msichana anaweza kusimamia afya yake ya hedhi kwa ubora na kujiamini.

Konferensi ya Waadventista wa Sabato ya Carolina huko Marekani inajumuisha majimbo ya Carolina Kaskazini na Kusini, yote yakiwa yamesheheni historia ya Marekani na kufahamika kwa maua yake, matunda na mashamba ya pamba. Watu wengi, wanapofikiria kuhusu Carolina, huona kina cha bluu-kijani cha Bahari ya Atlantiki ikizungukwa na mchanga mweupe wenye joto. Wengine huona siku za joto katika barabara pana zenye vivuli vya miti ya magnolia yenye maua meupe.

 

Ni wachache wanaokumbuka kwamba Carolina hufikia mbali katika milima mikubwa ya ukungu ambapo hali ya hewa mara nyingi ni baridi na theluji ni nyingi.

 

 

KUPANDA MLIMA

Ilikuwa Ijumaa ya joto mnamo Machi mwaka 1965, mwenyekiti wa konferensi Willard B. Johnson na mkewe Daisy walikuwa wakijiandaa kwa mwisho wa juma na washiriki wa kanisa katika mji wa Warrensville, mbali sana katika Nchi ya Northern High. Wakijua kuwa hali yao nzuri ya majira ya kuchipua inaweza kugeuka kuwa baridi na ya barafu katika milima, waliweka katika gari lao, mashuka ya joto, maji ya ziada na beleshi. “Endapo kungetokea chochote.

 

Bi. Johnson alihakikisha kuwa wanayo makoti mazito na glavu. “Huwezi kujua wakati ambapo theluji inaweza kushuka huko juu,” alimkumbusha Mchungaji Willard.

 

Usiwe na wasiwasi, alifikiri, huku akiweka mashuka na makoti kwenye kiti cha nyuma cha gari lao, kando tu ya kisanduku kidogo kilichokuwa na Biblia yake na maelezo ya hubiri.

Moja ya sehemu bora ya kuwa mwenyekiti wa konferensi ni kwamba unaweza kutembelea makanisa mengi tofauti, kushiriki habari njema za neema ya Mungu na marafiki Wakristo na kula chakula kitamu cha wenyeji. Mchungaji Willard na Daisy walikuwa wakiitazamia wikendi hii na hata walileta zawadi kadhaa kwa washiriki.

Huko nyumbani kwao Charlotte, Carolina Kaskazini, anga lilikuwa angavu, na vipimo vya joto vilitarajia wikendi yenye joto. Walipokuwa wakielekea kaskazini zaidi, hata hivyo, kulianza kuwa baridi zaidi. Mawingu yalilifunika kwa haraka jua na walilazimika kuwasha kikanza cha gari.

 

Kisha theluji ilianza kuanguka. Si sana, lakini ya kutosha kuwafanya watamani wangetoka mapema mchana.

 

Walizungumzia kuhusu kurudi na kuwapigia simu washiriki wa uteuzi wao wa Sabato, lakini waliamua kwamba Mungu kwa kweli aliwataka waendelee mbele, hata katika theluji inayoongezeka.

 

Ilikuwa rahisi kuendesha wakati theluji ilikuwa ikiyeyuka kwa haraka barabarani. Lakini ilikuwa vigumu zaidi wakati theluji ilifunika njia ya miguu na kuanza kuinamisha matawi ya miti chini.

 

Waliomba pamoja, wakimkumbusha Mungu kwamba walikuwa katika kazi Yake na kwamba walihitaji ulinzi Wake, wakimwomba Mungu awaongoze katika dhoruba na kuwaweka salama.

 

Punde theluji ilikuwa na kina cha zaidi ya inchi nne, ikiifunika barabara na kuifanya iwe ngumu kuona mahali ambapo barabara iliishia na mahali ambapo mtaro mpana ulianzia. Daisy na Mchungaji Willard walikumbuka kuwa waliwahi kupita katika barabara hii hapo kabla, lakini wakati huo walikuwa wanaweza kuona chini katika korongo refu kando ya barabara. Sasa walifikiria kuteleza kutoka barabarani na kupita upande katika kuta za korongo.

 

Waliomba zaidi, macho yao yakizama kwa umakini, wakijaribu kukaa kwenye viti vyao kwa uangalifu kama iwezekanavyo.

 

Dhoruba ilifunika mwanga wote na theluji ilituliza sauti zote. Walichoweza kusikia tu ilikuwa ni mngurumo wa injini ya gari na mapigo ya haraka ya mioyo yao.

 

 

NJE YA BARABARA

Hakukuwa na magari mengine barabarani na Mchungaji Willard alijitahidi sana kuendesha gari katikati ya barabara, lakini sasa theluji ilikuwa pana sana kiasi kwamba matairi yalionekana kwenda yalipotaka zaidi ya kule alikokuwa anayaelekeza. “Yalipotaka” ilikuwa zaidi na zaidi kuelekea upande wa korongo la barabara!

 

Kisha matairi ya upande wa kulia yakagonga ukingo wa njia ya miguu na gari likaingia kwenye mtaro mpana.

 

Mchungaji Willard alijaribu kuendesha gari mbele na nyuma, akitumaini kulipeleka kidogo kidogo kurudi juu ya njia ya miguu. Badala yake, gari liliteleza zaidi na zaidi mbali na barabara kuelekea kwa maafa. Kisha gari likasimama, likiwa limekwama katika theluji nene.

 

Waliomba tena. Kwa sauti tena. Pamoja tena. Kwa haraka wakimsihi Mungu kusitisha theluji, kulipatia gari nguvu zaidi na kumwambia kwamba “tafadhali tuma msaada!”

 

Kwa muda mrefu, hakuna kilichotokea. Kisha, polepole, dirisha la nyuma la gari lilianza kuonyesha mwanga wa njano kidogo.

 

“Kuna mtu anakuja!” Daisy alisema kwa kunong’oneza.

 

“Nadhani ndivyo,” Mchungaji Willard alijibu. Kisha akafungua mlango wake na kutoka nje kwenye barabara.

 

Mwanga uliongezeka wakati taa za mbele zenye kung’aa za Jeep Wrangler zilikaribia, aina ya gari ambalo ungelitarajia kulipata mahali ambapo barabara zilikuwa mbaya na hali ya hewa isiyotabirika. Jeep ilisimama kando yao na wanaume wawili wakubwa wa milimani waliokuwa wamevaa jinzi, kofia za joto, na makoti mazito, wakaja kando ya gari la Johnson.

 

 

“FUATA NYAYO ZETU”

Sasa, unahitaji kujua kwamba Mchungaji Willard alikuwa mtu mwenye mwili mkubwa sana, mwenye zaidi ya futi sita na uzito wa kutosha kuwa mchezaji hodari wa mpira wa miguu. Lakini, wakati wanaume wawili wa milimani walikutana na Mchungaji Willard katika theluji, walikuwa wakubwa sana kiasi kwamba Mchungaji Willard mwenye mwili mkubwa alionekana mdogo sana kando yao.

 

Wanaume wa milimani walicheka na kutabasamu walipovuta kwa mnyororo gari la Mchungaji.

 

“Jitayarishe kukanyaga mafuta,” mmoja wa wanaume alisema. “Tutakutoa katika mtaro na kukurudisha kwenye barabara.”

 

Mchungaji Willard alifuata maelekezo yao na punde Jeep hiyo ilikuwa ikitoa gari kutoka kwenye theluji nene na kulirudisha kwenye njia ya miguu. Baada ya muda mfupi walikuwa wamerudisha gari katikati ya barabara. Hata kama gari lilikuwa bado katika theluji, Daisy hatimaye aliachilia pumzi aliyokuwa akiizuia. Wanaume wa mlimani walitoa minyororo, wakawapungia mkono na kuanza kusema kwaheri.

 

“Bado msiondoke! Nahitaji kuwalipa kwa kazi yenu,” Mchungaji Willard alisema. “Mmeokoa uhai wetu!”

 

“Hakuna haja ya kutulipa,” walitabasamu na kucheka waliporudi kwenye Jeep yao. “Kukusaidia ilikuwa ndiyo furaha yetu! Sasa, endelea kufuata gari letu. Utaendesha kwa urahisi zaidi unapofuata mahali ambapo matairi yetu yamepita.”

 

Mchungaji Willard aliendesha kwa uangalifu sana, akifuata alama za matairi ya Jeep. Walipofika karibu na kona kubwa, Jeep ilikwenda mbali zaidi na zaidi mbele yao, na kisha ikatoweka kwenye dhoruba ya theluji. Mchungaji Willard aliendelea kuendesha kwa muda mrefu, macho yake yakiwa yamefungwa kwenye alama za Jeep ambazo ziliendelea katikati ya barabara.

Kisha alama zikapotea.

 

Mwanzoni Mchungaji Willard alikuwa na hofu, lakini akatulia alipoona taa dhaifu za mji mbele sana.

 

“Ilikuwa kama vile Jeep ilikuwa imeendeshwa kwenda juu angani,” Mchungaji Willard aliwaambia washiriki wa kanisa asubuhi iliyofuata. “Unajua,” aliongezea kwa tabasamu kubwa, “Tunadhani tunajua jinsi malaika wetu wanavyoonekana. Na hata tunajua aina ya gari wanaloliendesha.”

Katika mji wenye pilikapilika ambapo kulikuwa na majengo marefu yaliyopanda juu angani na honi za magari zisizokoma, aliishi mvulana jina lake Ethan. Ethan alikuwa mwenye umri wa miaka 10 na kama ilivyo kwa wavulana wengine wa umri wake, alipendelea burudani na safari kwenye maeneo ya kutisha.

 

Siku moja angavu na yenye jua, akitembea toka shuleni kwenda nyumbani, Ethan aliona kitu kikimetameta pembezoni mwa barabara. Kwa udadisi, aliinama chini na kugundua kuwa ni pochi ndogo ya kuwekea fedha, vitu vilivyokuwa humo vikijitokeza nje kidogo. Moyo wa Ethan ulidunda kwa msisimko alipoiokota pochi hiyo na kuitazama kwa karibu. Ilikuwa ni pochi ya ngozi, iliyochakaa kwa kukaa sana lakini bado ilikuwa imara, na ndani yake aliweza kuona kitita cha pesa, kadi fulani za benki, na leseni ya dereva.

 

Kwa muda mfupi, akili yake ilikimbia kwa mawazo ya kile ambacho angezifanyia fedha hizo. Alifikiria vitu vyote vya kuchezea ambavyo angejinunulia, burudani ambayo angeweza kuwa nayo bila mtu yeyote kujua fedha zilipotokea. Lakini baadaye, sauti ndogo ndani yake ilimnong’oneza, ikimkumbusha kuhusu aya ya Biblia iliyosomwa na familia yake katika ibada ya jioni iliyopita: “Aliye mwaminifu katika lililo dogo sana, huwa mwaminifu katika lililo kubwa pia; na aliye dhalimu katika lililo dogo, huwa dhalimu katika lililo kubwa pia” (Luka 16:10).

 

Akihisi kichomi cha hatia kwa wazo la kuificha pochi ile, Ethan alifanya uamuzi. Alijua alichotakiwa kufanya, hata kama haukuwa uamuzi rahisi kuufanya. Akiamua kwa kuitikia kwa kichwa, alikunja ile pochi vizuri na kuiweka kwenye begi lake sehemu ya nyuma, na kuendelea na safari kurudi nyumbani.

 

Ethan alipokuwa akitembea, hakuweza kujikwamua na hisia ya wasiwasi iliyokuwa katika tumbo lake. Pochi ilionekana kumletea mzigo akilini mwake, uwepo wake ukimkumbusha mara kwa mara uamuzi ambao alikuwa analazimika kuufanya. Lakini licha ya kushawishiwa kuitunza, Ethan alijua kwamba kufanya jambo sahihi kulikuwa muhimu zaidi kuliko raha ya muda mfupi ambayo pesa ingeweza kuleta.

 

Wakati Ethan alifika nyumbani, mara moja aliwaeleza wazazi wake kuhusu pochi aliyokuwa ameipata. Pamoja, walikagua kwa uangalifu vilivyokuwa ndani yake na kujadili watakachokifanya baadaye. Wazazi wa Ethan walimpongeza kwa uaminifu wake, wakimkumbusha kwamba kuchagua kufanya jambo sahihi, hata kama ilikuwa ni vigumu, ilikuwa njia bora ya kuifuata daima.

 

Siku iliyofuata, Ethan na wazazi wake walikwenda kwenye kituo cha polisi ili kuisalimisha pochi. Walipokaribia meza ya mbele, Ethan alihisi wimbi la wasiwasi likimjia. Itakuwaje endapo mtu aliyepoteza pochi angemkasirikia kwa kuitunza? Itakuwaje endapo wangemshutumu kwa kuchukua pesa?

 

Ethan alipokabidhi pochi kwa afisa wa zamu na kueleza jinsi alivyoipata, hofu zake zote zilipotea. Afisa alimshukuru kwa uaminifu wake na kumhakikishia kwamba wangefanya kila wawezalo kumrudishia mmiliki halali.

 

Ethan alipotoka kwenya kituo cha polisi, hali ya amani ilimjia. Alijua kwamba alikuwa amefanya jambo sahihi na hilo ndilo lililokuwa la muhimu. Akitafakari juu ya uzoefu wake, Ethan hakuweza kuacha kufikiria kuhusu kisa alichowahi kukisikia katika Shule ya Sabato kuhusu mtu aliyeitwa Yusufu.

 

Yusufu alikabili taabu nyingi na majaribu, lakini daima alibakia kuwa mwaminifu kwa jambo lililo sahihi. Hata alipofungwa gerezani kwa kosa ambalo hakuwa amelitenda, Yusufu alimtegemea Mungu na kubaki thabiti katika haki yake. Na mwishowe, uaminifu wake ulipata thawabu, na akapewa cheo kikubwa na jukumu kubwa.

 

Kama Yusufu, Ethan alikabiliana na uchaguzi mgumu, lakini alikuwa amechagua kufanya jambo lililo sahihi, hata kama lilikuwa gumu. Na alijua kwamba mwishowe uaminifu wake ungepata thawabu—kwa njia fulani.

 

Siku kadhaa zilipita, na Ethan akaanza kujiuliza kilichotokea kwa pochi. Je, polisi walimpata mmiliki?

 

Jioni moja, palibishwa hodi katika mlango wa mbele. Mama ya Ethan alifungua, akazungumza na mtu kwa muda, kisha akamwita Ethan aje. Kwa hamu, aliizunguka kona ya jikoni na kumwona mtu aliyesimama pale, kofia yake ikiwa mikononi.

“Je, wewe ndiye Ethan?” mtu huyo aliuliza.

“Ndiyo, mimi ndiye,” Ethan alijibu, akiwa na mchanganyiko wa wasiwasi na taharuki.

 

Mtu huyo alitabasamu na kumnyooshea mkono wake. “Mimi ni John,” alisema. “Mimi ndiye niliyepoteza pochi uliyoiokota. Siwezi kukushukuru vya kutosha kwa kunirudishia.”

Moyo wa Ethan ulijawa fahari wakati John alipoeleza jinsi pochi ilivyokuwa ya muhimu kwake. Ilikuwa ni ya baba yake na ilikuwa na thamani ya muhimu zaidi ya fedha zilizokuwemo ndani. John alisisitiza kumpatia zawadi Ethan kwa uaminifu wake, lakini Ethan alikataa kwa upole, akijua kwamba tayari alikuwa ameshapata thawabu kwa njia bora zaidi—kwa kufanya lililo sahihi.

 

John alipokuwa anaondoka, Ethan hakuweza kujizuia kuhisi hisia ya kuridhika. Alikuwa amekabili uchaguzi mgumu na alikuwa amechagua kufanya lililo sahihi, hata wakati ilikuwa vigumu. Na mwishowe, uaminifu wake ulipata thawabu, si tu kwa shukrani za mgeni, bali pia kwa kujua kwamba alikuwa amemheshimu Mungu.

 

Tangu siku hiyo, kila Ethan alipokabiliana na majaribu au uamuzi mgumu, alikumbuka kisa cha Yusufu na somo alilojifunza. Alikuwa anajua kwamba kama angebakia imara katika ahadi yake ya kumtii Mungu na kumtegemea kwenye mpango Wake, daima angepata nguvu ya kufanya lililo sahihi.

Mchapishaji

Jarida la Adventist World, jarida la kimataifa la Kanisa la Waadventista wa Sabato. Konferensi Kuu, Divisheni ya Asia Pasifiki ya Waadventista wa Sabato ndio wachapishaji.

 

Mkurugenzi Mtendaji/ Mkurugenzi wa Huduma za Adventist Review

Justin Kim

 

Meneja wa Uchapishaji wa Kimataifa

Hong, Myung Kwan

 

Kamati ya Uratibu ya Jarida la Adventist World

Yo Han Kim (chair), Tae Seung Kim, Hiroshi Yamaji, Myung Kwan Hong, Seong Jun Byun, Dong Jin Lyu

 

Wakurugenzi wenza/ Wakurugenzi, Huduma za Adventist Review

Sikhululekile Daco, John Peckham, Greg Scott

 

Wahariri waliopo Silver Springs, Maryland, Marekani

Enno Müller, Beth Thomas

 

Wahariri waliopo Seoul Korea
Hong, Myung Kwan; Park, Jae Man; Kim, Hyo-Jun

 

Mkurugenzi wa Mambo ya Kidijitali

Gabriel Begle

 

Mkurugenzi wa Muungano wa Mifumo na Uvumbuzi

Daniel Bruneau

 

Meneja wa Shughuli

Merle Poirier

 

Mratibu wa Tathmini ya Uhariri

Marvene Thorpe-Baptiste

 

Wahariri /Washauri wengine

E. Edward Zinke

 

Meneja wa Fedha

Kimberly Brown

 

Mratibu wa Usambazaji

Sharon Tennyson

 

Mratibu wa toleo la Kanda (Adventist World)

Penny Brink

 

Bodi ya Utawala

Yo Han Kim, chair; Justin Kim, secretary; Hong, Myung Kwan; Karnik Doukmetzian; SeongJun Byun; Hiroshi Yamaji; Joel Tompkins; Ray Wahlen; Ex-officio: Paul H. Douglas; Erton Köhler; Ted N. C. Wilson

 

Maelekezo ya Usanifu na Muundo

Types & Symbols

 

Kamati ya Adventist World ya Divisheni ya Afrika Mashariki – Kati:

Blasious Ruguri, Musa Gideon Mitekaro, Tom Ogal, Emanuel Pelote.

 

Tafsiri

Ufunuo Publishing House, South Tanzania Union Conference.

 

Msomaji wa prufu

Lilian Mweresa

 

Usanifu wa toleo la Kiswahili

Daniella Batista, Ashleigh Morton, Digital Publications

 

Uchapishaji wa Kidijitali

Charles Burman, Digital Publications (www.digitalpublications.co.za)

 

Muelekeo wa Sanaa na Ubunifu

Mark Cook, Brett Meliti, Ivan Ruiz-Knott

/Types & Symbols

 

Kwa Waandishi: Tunakaribisha miswada huria. Tuma barua zote kwa uhariri kwa 12501 Old Columbia Pike, Silver Spring, MD 20904-6600, U.S.A. Faksi ya ofisi ya Uhariri ni: (301) 680-6638

 

Waraka pepe: worldeditor@gc.adventist.org

Tovuti: www.adventistworld.org

 

Rejea zote za Biblia zimechukuliwa kutoka kwenye Swahili Union Version Bible Toleo la Chama cha Biblia la mwaka 1952.

 

Jarida la Adventist World linachapishwa kila mwezi na kuchapwa kwa wakati huo huo huko Korea, Brazili, Indonesia, Australia, Ujerumani, Austria, Ajentina, Meksiko, Afrika Kusini, na Marekani.

 

Vol. 20, Na. 5

Swipe left

swipe left To move to the next page

Swipe right

swipe right To move to the previous page
Allow Send-it to use cookies?

Send-it uses cookies to track how you use the application. Find out more about what data we collect and how we use the data in our privacy policy.